1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya kujadili juu ya kuifunga mipaka

Sylvia Mwehozi
17 Machi 2020

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanapanga kufanya mkutano wa pili wa kilele siku ya Jumanne katika kipindi cha wiki mbili, katika jaribio la kuunda jitihada za pamoja za kukabiliana na mripuko wa virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3ZYpN
Italien Castelpusterlengo, Lombardei | Coronavirus | Straßensperre, Soldat mit Atemschutz
Picha: picture-alliance/Photoshot

Maambukizi ya  virusi hivyo barani Ulaya yamepindukia watu  50,000 na zaidi ya watu 2000 wamepoteza maisha. Maambukizi ya virusi hivyo yameathiri masoko na kusababisha hofu kwa umma, lakini serikali zimeanzisha hatua za haraka, ikiwemo kuifunga baadhi ya mipaka yake au kuwaweka watu karantini.

Baada ya Italia kuchukua hatua za kuwafungia raia wake kutokana na COVID-19, Uhispania na sasa Ufaransa, zote zimeanzisha hatua za kuwafungia watu nyumbani isipokuwa tu kwa shughuli za dharura kama vile kununua chakula au kuelekea hospitali. Nchi saba zimeiarifu Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, kwamba zimeanzisha ukaguzi wa vitambulisho ndani ya maeneo kunakoruhusiwa pasipoti za Schengen. Miongoni mwa nchi hizo ni Austria, Hungary, Jamhuri ya Czech na Poland, ambazo zote zilichukua hatua za upande mmoja za kuzuia wimbi la wakimbizi mwaka 2015.

Brüssel | Pressekonferenz Ursula von der Leyen und Charles Michel nach Treffen mit Erdogan
Rais wa Halmashauri ya Ulaya Ursula von der Leyen na rais wa baraza la Ulaya Charles Michel Picha: Reuters/F. Lenoir

Alipoulizwa jana Jumatatu endapo Ulaya inaweza kurejea kwenye ukaguzi halisi wa vitambulisho baada ya hili, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema "Natumai hivyo, lakini imeonyeshwa dhahiri kwamba utaratibu huo haukufanya kazi vizuri katika njia ambayo mtu alitegemea". Tatizo kubwa linalowakabili vongozi wanapokutana kufanya mkutano kwa njia ya vidio ni namna ya kukomesha maambukizi mapya ya virusi vya corona, kushirikiana katika kuifunga mipaka na kuhakikisha kwamba vifaa muhimu vya tiba na vyakula vinaweza kuwafikia wale walio na uhitaji.

Viongozi hao pia wanatarajiwa kuanzisha marufuku ya siku 30 ya kusafiri kwa watu wanaotaka kuingia Ulaya hasa kwa shughuli za Utalii na biashara nyingine. Wale walio na ukaazi wakudumu, wanadiplomasia, wafanyakzi wa afya na usafiri hao hawatoguswa na katazo hilo. Pia kunatarajiwa kuanzishwa njia ya kijani ndani ya mipaka ya Ulaya ili kuwezesha magari yaliyobeba vifaa maalumu kuepukana na msongamano wa magari ambao umeanza kujitokeza katika maeneo ya kuvuka.

Kusudio kuu kwa mujibu wa rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel ambaye ataongoza mkutano wa Jumanne ni "kupunguza safari zisizo kuwa na umuhimu lakini pia wakati huo huo kuwezesha usambazaji wa bidhaa, ili kuweza kuhakikisha haraka inavyowezekana uadilifu wa soko la pamoja, na kuhakikisha usambazaji wa bidhaa zinazohitajika."