1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJordan

Mkutano wa kilele wa Mashariki ya kati kufanyika Jordan

20 Desemba 2022

Mashariki ya kati inashuhudia migogoro tangu ya kiuchumi,mpaka kisiasa na mkutano wa Jordan unalenga kutafuta ufumbuzi wa migogoro hiyo

https://p.dw.com/p/4LF6C
Jordanien Nahost-Gipfel in Amman | Abdel Fattah al-Sisi
Picha: Yousef Allan/Jordanian Royal Palace/AFP

Viongozi wa mashariki ya kati wanakutana leo Jumanne nchini Jordan katika mkutano wao wa kilele unaowaleta pamoja viongozi wenye usemi wa  kikanda na kimataifa,yakiwepo matumaini wa kupatikana mwafaka kutatuta migogoro ya kikanda na hasa mgogoro wa Iraq.

Mkutano huu uliopewa jina la Badhdad nambari mbili ambao pia utawajumuisha maafisa kutoka Ufaransa na Umoja wa Ulaya unafuatia mkutano mwengine wa kilele uliofanyika mwezi Agosti mwaka jana katika mji mkuu wa Iraq ulioandaliwa kwa juhudi zilizoanzishwa na  rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Hali ya Iraq

Ikumbukwe kwamba Iraq iliifikia katika makubaliano tete ya kuunda serikali baada ya kushuhudiwa mwaka mzima wa mkwamo wa kisiasa.

Na taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais wa Ufaransa imesema mkutano unaofanyika katika pwani ya bahari ya chumvi  unalenga kutoa mchango wa kusaidia kuleta uthabiti,usalama na ufanisi kwa Iraq.

Jordanien Nahost-Gipfel in Amman | Mohamed Shia al-Sudani
Picha: Yousef Allan/Jordanian Royal Palace/AFP

Ofisi ya rais Macron pia imeongeza kusema kwamba inataraji mkutano huu utakuwa wa manufaa kwa kanda nzima.

Kadhalika mkutano huu unafanyika katika wakati ambapo nchi nyingi katika kanda ya Mashariki ya Kati zimegubikwa na migogoro.

Kwa kipindi cha zaidi ya miezi mitatu ,Iran imekuwa ikishuhudiwa matukio ya ukandamizaji ya  umwagaji damu yanayofanywa dhidi ya watu wanaofanya maandamano yaliyochochewa na kifo cha msichana Mahsa Amin mnamo Septemba 16.

Msichana huyo wa miaka 22 mwenye asili ya kikurdi   alikufa akiwa mikononi mwa polisi wa maadili wa Iran. Mkutano huo pia utahudhuriwa na mwanadiplomasia wa ngazi ya juu katika Umoja wa Ulaya Joseph Borrell ambaye amekuwa akisimamia mazungumzo ya usuluhishi yanayolenga  kufufua makubaliano ya Nyuklia ya Iran na nchi zenye nguvu duniani.

Syria ni nchi nyingine inayoendelea kushuhudia vita ikiwa ni uwanja wa mapambano ya kuwania maslahi ya siasa za kieneo  pamoja na Lebanon ambayo imebakia katika mkwamo mkubwa wa kiuchumi na kisiasa.

Biden aondoka Saudi Arabia baada ya kukamilisha ziara yake ya kwanza ya Mashariki ya Kati kama Rais

Mkutano wa Baghadad nambari mbili  unaofanyika Jordan utahudhuriwa pia na waziri mkuu mpya wa Iraq  Mohammed Shia al-Sudani,waziri wa mambo ya nje wa Iran na wajumbe kutoka Uturuki na Saudi Arabia.

Jordanien Nahost-Gipfel in Amman | Abdel Fattah al-Sisi
Picha: Yousef Allan/Jordanian Royal Palace/AFP

Jordan ambayo imeshuhudia migomo na maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta katika siku za hivi karibuni  imeshasema kwamba jeshi limetawanywa katika barabara za kuanzia uwanja wa ndege wa Amman  hadi kwenye eneo la mkutano huo katika pwani ya bahari ya chumvi ,ambako ni kiasi kilomita 50 kutoka magharibi mwa mji mkuu huo wa Jordan.

Wachambuzi kama Riad Kahwaji ambaye ni mkurugenzi wa taasisiinayohusika na masuala ya kijeshi ya mashariki ya kati na ghuba anasema mkutano huo una malengo makubwa lakini hakuna anayetarajia miujiza.

Kahwaji anasema Ufaransa katika nafasi yake kama msuluhishi  ni muhimu huku nchi hiyo ikiendeleza mdahalo na Iran kwa niaba ya nchi za Magharibi  na hasa kwakuwa mazungumzo ya Vienna kwahivi sasa yamekwama.

Mchambuzi huyo mwenye makaazi yake Dubai anasema ni muhimu kuutambua msimamo wa Iran ambayo inabeba dhima kubwa katika migogoro ya kanda hiyo kuanzia Iraq hadi Syria kwenda Lebanon mpaka Yemen,ili kufikia maelewano ya pamoja.

Nchi za kiarabu zaahidi kuendelea kuiunga mkono Palestina

Jordanien Nahost-Gipfel in Amman | Josep Borrell und Hossein Amir-Abdollahian
Picha: Iranian Foreign Ministry/AFP

Na sio hilo tu,Kahwaji anasema pia mchango wa Iran katika mgogoro wa Ukraine kupitia hatua yake ya kupeleka droni kwa Urusi  inazidi kuleta mkanganyiko katika mazungumzo.

Ikumbukwe Iran imeishutumu hasimu wake katika kanda hiyo Saudi Arabia Saudi Arabia ambayo haina  mahusiano nayo ya kidiplomasia tangu mwaka 2016,kwamba ndiyo inayochochea machafuko ndani ya Iran wakati yakishuhudiwa maandamano. Siku ya Jumatatu Ilitajwa kwamba Iran imesema iko tayari kurudisha mahusiano ya kidiplomasia na Riyadh pale Saudi Arabia itakapokuwa tayari.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW