1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Ujumbe wa ECOWAS hauwezi kupokewa Niger kwasababu ya usalama

8 Agosti 2023

Viongozi wa mapinduzi nchini Niger wameiambia Jumuiya ya ECOWAS kwamba hawawezi kupokea ujumbe uliopendekezwa mjini Niamey kwa sababu za kiusalama

https://p.dw.com/p/4UvG7
Washiriki wa mkutano wa ECOWAS mjini Abuja, Nigeria mnamo Julai 30, 2023
Washiriki wa mkutano wa ECOWAS mjini Abuja, Nigeria mnamo Julai 30, 2023Picha: Xinhua News Agency/picture alliance

Katika barua kwa wawakilishi wa ECOWAS mjini Niamey, wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imesema kuwa mazingira ya sasa na uasi kufuatia vikwazo vilivyowekwa na ECOWAS hayaruhusu kukaribishwa kwa ujumbe huo katika mazingira yanayohitajika ya utulivu na usalama. Barua ya viongozi hao wa mapinduzi iliyotolewa jana, imesema kuwa kuahirishwa kwa ziara ya wajumbe hao mjini Niamey ni muhimu kama ilivyo kufanyia kazi upya baadhi ya masuala katika ratiba ya wajumbe hao. Ratiba hiyo inajumuisha mikutano na baadhi ya watu maarufu ambayo haiwezi kutekelezwa kwa sababu wazi za kiusalama kutokana na mazingira ya tishio la uchokozi dhidi ya Niger. ECOWAS imeweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Niger baada ya wanajeshi waasi kuipindua serikali ya rais Mohamed Bazoum, mnamo Julai 26. Jumuiya hiyo pia ilitoa muda wa mwisho ambao ulikamilika siku ya Jumapili kumrejesha madarakani Bazoum ama kukabiliwa na athari ya matumizi ya nguvu.

Macron asema ni jukumu la ECOWAS kufanya maamuzi kuhusu Niger

Katika hatua nyingine, serikali ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron inaamini kuwa ni jukumu la ECOWAS kufanya maamuzi kuhusu jinsi ya kudumisha utaratibu wa kikatiba nchini Niger. Haya ni kwa mujibu wa chanzo kimoja cha kidiplomasia ambacho hakikutambulishwa.

Viongozi wa mapinduzi nchini Niger wakihudhuria mkutano wa hadhara katika uwanja mmoja mjini Niamey, Agosti 6 2023
Viongozi wa mapinduzi nchini Niger wakihudhuria mkutano wa hadhara katika uwanja mmoja mjini Niamey, Agosti 6 2023Picha: Mahamadou Hamidou/REUTERS

Chanzo hicho kimesema kuwa kama washirika wao wote, wanaunga mkono kikamilifu juhudi za mataifa ya kikanda za kudumisha demokrasia nchini Niger. Viongozi wa mataifa ya Magharibi wanatarajiwa kufanya mkutano wiki hii kuhusu mzozo nchini Niger baada ya viongozi wa kijeshi nchini humo kukaidi muda uliowekwa wa kurejesha madarakani serikali iliyochaguliwa kikatiba ama kukabiliwa na muingilio wa kijeshi.

Jumuiya ya ECOWAS kukutana  mjini Abuja siku ya Alhamisi

Katika majibu yake ya kwanza rasmi tangu viongozi hao wa kijeshi walipopuuza muda huo wa mwisho wa Jumapili wa kumrejesha madaraka rais Bazoum, Jumuiya ya ECOWAS imesema itakutana mjini Abuja siku ya Alhamisi. Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Catherine Colonna, amesema Bazoum na serikali yake iliyoondolewa madarakani, ndio mamlaka ya kipekee halali ya Niger. Afisa mmoja wa wizara hiyo ya Ufaransa ameongeza kuwa Ufaransa inaunga mkono kwa nguvu zote juhudi za kubatilisha mapinduzi hayo ya kijeshi. Chanzo kilicho karibu na ECOWAS kimesema uingiliaji wa kijeshi wa mara moja wa kumrejesha Bazoum madarakani hautarajiwi kwa wakati huu na kuongeza kuwa njia ya mazungumzo bado inaonekana kuwa wazi.