1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Viongozi wa Afrika wahimiza amani kati ya Ukraine na Urusi

16 Juni 2023

Ujumbe wa wakuu wa mataifa ya Afrika umefanya ziara nchini Ukraine kuhimiza amani kati ya Ukraine na Urusi, na kuhakikisha ugavi wa chakula na mbolea kwa bara lao, lakini ziara hiyo imetikiswa na mashambulizi mjini Kyiv.

https://p.dw.com/p/4ShEU
Ukraine | Afrikanische Delegation in Bucha
Picha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Ujumbe huo wa amani, ukihusisha viongozi kutoka Afrika Kusini, Senegal, Zambia, Comoro an Misri, wamekutana na wawakilishi wa wizara ya ulinzi kabla ya mazungumzo yaliopangwa baadae Ijumaa na rais Volodymyr Zelenskiy.

Viongozi hao wanatazamiwa kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini St Petersburg siku ya Jumamosi na, wakati Kyiv na Moscow zikichuana kyashawishi mataifa ya ulimwengu wa tatu, wanaona fursa ya kupatanisha katika vita ambavyo vimeziathiri nchi za Afrika kwa kuvuruga ugavi wa nafaka na chakula kingine.

Viongozi hao wa Kiafrika, wakiwemo maraisa wa Afrika Kusni Cyril Ramaphosa, na wa Senegal Macky Sall, walianza ziara yao kwa kuutembelea mji wa Bucha ulioko nje ya Kyiv, ambako Ukraine inaishtumu Urusi kufanya mauaji, ubakaji na mateso wakati vikosi vyaka vilipoukalia mji huo. Wachunguzi wa kimataifa wanakusanya ushahidi wa uhalifu wa kivita mjini Bucha, inagwa Urusi inakanusha madai hayo.

Viongozi wa Afrika wataka kumaliza mzozo wa Ukraine

Wakiwa ndani ya Kanisa la Mtakatifu Andrew la Bucha, viongozi hao walitazama onyesho la picha za kugofya za miili iliyopatikana ikiwa imelala mitaani Machi mwaka jana, siku chache baada ya wanajeshi wa Urusi kufurushwa na vikosi vya Ukraine.

Soma pia: Ujumbe wa viongozi wa Afrika wawasili Ukraine

Mamia ya raia walikusanywa na kuuawa kwa kupigwa risasi au kuchinjwa katika mji huo, ambao jina lake limekuja kulinganishwa na maovu makubwa yaliofanywa na vikosi vya Urusi katika vita vya karibu miezi 16 vilivyoanzishwa na Rais Putin nchini Ukraine.

Wahimiza kulinswa kwa maisha ya watu wote

Rais Ramaphosa alimuambia mwendesha mashtaka mkuu wa Ukraine Andriy Kostin baada ya viongozi hao kuweka mishumaa ya kumbukumbu katika kituo cha kumbukumbu kilichopo nje ya kanisa, kwamba kifo cha yeyote kinatupunguza sote.

Naye rais wa Zambia Hakainde Hichilema akaongeza kuwa laazima maisha ya watu wa Ukraine yalindwe kama haki ya msingi. "Maisha ni ya ulimwengu wote, na lazima tulinde maisha - maisha ya wa Ukraine, maisha ya Warusi, maisha ya ulimwengu," alisema rais Hichilema.

Afrikanische Staats- und Regierungschefs reisen auf einer Friedensmission in die Ukraine
Viongozi wa mataifa ya Afrika wakiwa njiani kwenda Kyiv kwa usafiri wa treni wakitoeka Warsaw, Poland, Juni 16, 2023.Picha: REUTERS

"Hilo ni muhimu. Hivyo lindeni maisha, na kuzingatia maendeleo. Kukosekana kwa utulivu popote ni kutokuwa na utulivu kila mahali. Ubinadamu ni mmoja. Hivyo basi, lazima sote tuzingatie amani, usalama na utulivu na kujikita kwenye maendeleo."

Soma pia:Ukraine yadai kupata mafanikio uwanja wa mapambano 

Rasimu ya waraka ulioonekana na Reuters inasema lengo la ujumbe wa viongozi wa Afrika ni kukuza amani na kuhimiza pande husika kukubaliana na mchakato unaoongozwa na diplomasia. Mataifa ya Afrika yameathirika pakubwa na  vita hivyo, ambavyo vimeongeza mfumuko wa bei za vyakula na kuzidisha majanga ya njaa.

Ziara ya viongozi hao imejiri wakati Ukraine imeanzisha kampeni kubwa ya mashambulizi kurejesha maeneo yanayokaliwa na vikosi vya Urusi mashariki na kusini mwa nchi hiyo,  ambayo Rais  wa Urusi Vladmir Putin amesema haitafua dafu, na kudai kuwa vikosi vya Ukraine vilikuwa vinapata hasara kubwa katika uwanja wa mapambano.

Chanzo: Mashirika