1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi Boko Haram waingizwa orodha ya magaidi

22 Juni 2012

Marekani kwa mara ya kwanza imewaweka viongozi watatu wanatuhumiwa kuongoza kundi la Boko Haram lililopo eneo la Maiduguri, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, katika orodha ya magaidi wa Kimataifa.

https://p.dw.com/p/15K4A
Kiongozi wa Boko Haram
Kiongozi wa Boko HaramPicha: AP

Viongozi hao ni Abubakar Shekau, ambaye yeye mwenyewe alijitangaza kuwa analiongoza kundi hilo akiwa na ushirikiano wa karibu na kikundi cha Al-Qaeda. Wengine ni Abubakar Adam Kambar na Khalid al Barnawi.

Boko haram maana yake elimu za magharibi ni dhambi

Kikundi hiki kilianza harakati zake mwaka 2003 na mwaka mmoja baadae kilifanya shambulio la kwanza. Huku jina la kundi hili lina maana ya elimu za magharibi ni dhambi.

Wanamgambo hao wanapenda kuvaa mavazi kama yale ya kikundi cha Taliban vilembe kichwani na kufuga ndevu nyingi. Madai ya kundi hili ni kutaka kuanza kutumika sheria ya dini ya kiislamu, shariah, katika taifa zima la Nigeria lenye lenye waislamu na wakristo.

Mojawapo ya eneo la Kano lililoshambuliwa na Boko Haram
Mojawapo ya eneo la Kano lililoshambuliwa na Boko HaramPicha: picture-alliance/dpa

Kiongozi wa zamani alipigwa risasi

Mwaka 2009, kiongozi wa zamani wa kundi hili, Mohammed Yusuf, alipigwa risasi akiwa korokoroni na kuuwawa baada ya kusabisha mauwaji ya watu 800 katika mapigano na vikosi vya usalama vya nchi hiyo.

Akilitazama tatizo hilo nchini kwake, Rais Goodluck Jonathan, alipokuwa anakaribisha mazungumzo na Boko Haram, alisema,"mazungumzo haya lazima yafanyike tena sasa, na lazima tupambane na ugaidi kwa mbinu zote, kwani mazumgumzo na magaidi hayawezi kumaliza ugaidi."

Mauwaji mengine ya kutisha yalifanywa na kundi hili Januari 2012 katika eneo la Kano, na kusababisha watu 186 kufariki. Shambulio hilo lilitanguliwa na shambaulio lingine katika makazi ya Umoja wa mataifa huko Abuja na kusababisha vifo vya watu 23 agosti mwaka 2011.

Taarifa ya Human rights watch

Kulingana na taarifa za Shirika la Haki za Binadamu la Human right Watch, limesema watu 935 wameuwawa na kundi hili tangu mwaka 2009. Pia limekuwa likilenga makanisa mathalani mashambulio katika siku ya noeli na pasaka ambayo yalisababisha vifo vya watu wengi.

Aprili 29 mwaka huu, katika eneo la Maiduguri, ambalo ndipo makazi ya wanamgambo hawa, mtu mmoja aliyekuwa na bunduki aliwashambulia waumini19 wa kikristo. Siku mbili baadae mtuhumiwa huyo alikamatwa mjini Kano.

Kauli ya kiongozi wa kundi hilo

Kiongozi wa kundi hilo Abubakar Shekau akizungumzia kauli ya serikali ya Nigeria kupambana na ugaidi na kupambana nao alisema "hakuna mtu asiyeamini katika Mungu wa kweli anaweza kusema juu yetu, tunaamini katika Mungu, tunamwambia Rais Jonathan hawezi kutufanya lolote kama Mungu hapendi na kwa kweli hatuogopi kufa."

Askari wa Nigeria wakiwa katika mapambano na Boko Haram
Askari wa Nigeria wakiwa katika mapambano na Boko HaramPicha: dapd

Mei 2 mwaka huu, mtu mwingine mwenye silaha aliwauwa watu 56 katika mji wa Potiskum, katika jimbo la Yobe, ambapo polisi wa jimbo hilo walithibitisha vifo vya watu hao na kulihusisha tena kundi la Boko Haram.

Bomu la kujitolea mhanga kanisani liliripuka tena katika mji wa Yelwa, karibu na viunga vya Bauchi, Juni 3. Siku saba baadae watu watatu wenye silaha waliwavurumushia risasi waumini wa kikristo waliokuwepo kanisani katika mji wa Biu, katika jimbo la Borno

Mwandishi:Adeladius Makwega/RTRE

Mhariri: Miraji Othman