1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Israel vyaendelea kuushambulia Ukanda wa Gaza

Sylvia Mwehozi
19 Julai 2024

Vikosi vya Israel vimeyashambulia maeneo ya katikati mwa Gaza leo, na kuwauwa Wapalestina wanane katika kambi ya Al-Nuseirat.

https://p.dw.com/p/4iWUv
Ukanda wa Gaza | Athari za mashambulizi ya Israel
Taathira za mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: EYAD BABA/AFP/Getty Images

Mapigano pia yameripotiwa kupamba moto katika mji wa kusini wa Rafah ambako mamlaka za afya zimesema raia wengine watano wameuawa.

Wapalestina walioko eneo salama la Al-Mawasi katika mji wa Khan Younis, wameelezea hofu kutokana na mashambulizi mabaya ya Israel, wakisema hakuna eneo salama ndani ya ukanda huo. Eneo hilo linawahifadhi Wapalestina waliokimbia mapigano kutoka maeneo mengine ya Gaza.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, atakayelihutubia Bunge la Marekani wiki ijayo, alifanya ziara ya kushtukiza katika eneo la karibu na Rafah siku ya Alhamis.

Netanyahu aliwaeleza wanajeshi wa Israel, kuwa shinikizo la kijeshi pamoja na madai ya kuwarejesha mateka 120 ambao bado wanashikiliwa Gaza yanaonekana kuzaa matunda.