1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vijana mjini Beni washika Doria kufuatia ongezeko la uhalifu

John Kanyunyu10 Septemba 2021

Baadhi ya vijana wa kata ya Kalinda mjini Beni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekuwa wakishika doria usiku katika mji huo kufuatia ongezeko la visa vya uhalifu lakini wametimuliwa na polisi.

https://p.dw.com/p/409ar
Demokratische Republik Kongo Beni
Picha: Imago Images/Afrikimages/K. Musayi

Hatua ya vijana kushika doria katika kata ya Kalinda inafuatia malalamiko ya wakaazi wa Beni kutokana na uporaji mali usiku unaodaiwa kufanywa na watu wanaobeba silaha.

Uporaji huo unatokea katika wakati ambapo hali ya dharura inatekelezwa katika mikoa ya Kivu ya Kaskazini pamoja na Ituri, huku wakaazi wa mikoa hiyo wakizuiwa kutoka nje ifikapo saa tatu za usiku. Vijana hao wanaoshika doria wamelaani ongezeko la visa vya ujambazi na wameahidi kulinda mali zao usiku.

Msemaji wa polisi katika mji wa Beni Nasson Murara ameiambia DW kwamba, polisi iliwatawanya vijana waliokuwa wanaandamana kulalamikia ukosefu wa usalama japo hivi sasa hali ya utulivu imerudi. 

Maandamano ya mjini Beni, ni ya pili kufanyika tangu kutangazwa kwa hali ya dharura katika eneo hili. 

Wakaazi pamoja na wabunge waliokuwa wanadhani kwamba hali ya usalama itaboreka wakati huu wa hali ya dharura, wameonyesha masikitiko yao kwani hali ya usalama imezidi kuzorota tofauti na hali ilivyokuwa kabla ya kutangazwa kwa hali ya dharura yapata miezi minne iliyopita.

Deutschland | G20 | Compact with Africa meeting in Berlin | Felix Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix TshisekediPicha: Tobias Schwarz/REUTERS

Na ili kutathmini hali ya operesheni za kijeshi wilaya ya Beni, mwakilishi maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Monusco, bi Bintou Keita amewasili Beni, ambako alifanya mazungumzo na kamanda wa jeshi la Congo Brigedia Mputela Bertin.

Baada ya mazungumzo yao, Bintou Keita alisema...

"Tulijadili masuala yanayopaswa kufanikisha hali ya dharura na kwaajili ya hiyo tulifikiria kwa pamoja jinsi ya kuendesha operesheni hizo hasa katika ususiano baina ya jeshi la Congo FARDC na Monusco. Tuligusia pia mambo ambayo tunapashwa kuboresha kwa pande zote mbili ilitufikie ushindi wa operesheni."

Hali ya usalama katika mji wa Beni, wilaya za Beni pamoja na Irumu inaendelea kuzorota wakati zikiwa zimesalia siku tano tu kabla ya wabunge kujadili uwezekano wa kuongoza muda zaidi kwa hali ya dharura.

Watu zaidi ya mia tano wameuawa tangu kutangazwa kwa hali ya dharura katika mikoa ya Kivu ya Kaskazini pamoja na Ituri huku matumaini ya kuona mauwaji na visa vya uhalifu vinakomeshwa, yakizidi kudidimia.