1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vienna. Iran inaweza kuwekewa vikwazo.

3 Septemba 2005
https://p.dw.com/p/CEew

Shirika la kimataifa la nishati ya kinuklia , IAEA limethibitisha kuwa Iran imeshindwa kuacha kazi ya kusafisha mafuta ya kinuklia , katika ripoti ambayo imesema maswali kadha yanabaki bila majibu juu ya mpango wake huo.

Ugunduzi huo unaweza kuzusha nchi hiyo kuwekewa vikwazo vya baraza la usalama la umoja wa mataifa kuhusiana na kitisho kuwa Iran inatengeneza silaha za kinuklia.

Baada ya miaka miwili na nusu , shirika hilo la kinuklia lenye makao yake makuu mjini Vienna limesema haliko bado katika nafasi ya kufafanua baadhi ya masuala muhimu ya kusafisha mafuta ya kinuklia ambayo ni hatua muhimu kuelekea kurutubisha madini ya Uranium.

Mkuu wa idara ya sera za nje wa umoja wa Ulaya Javier Solana amesema siku ya Alhamis kuwa umoja wa Ulaya uko tayari kwenda katika baraza la usalama la umoja wa mataifa kwa ajili ya kuiwekea vikwazo Iran kama haitakubaliana na wito wa shirika hilo la kimataifa la kinuklia kuacha kazi ya kusafisha mafuta hayo ya kinuklia.