1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

VIENNA: IAEA yasema Iran imeendelea kurutubisha uranium

1 Septemba 2006
https://p.dw.com/p/CDGG

Muda uliotolewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa Iran kusitisha harakati zake za kinuklia umemalizika,bila ya kuwepo ishara ya kupatikana suluhisho.Ripoti iliyotolewa na Shirika la Nishati ya Kinuklia la Umoja wa Mataifa-IAEA,mjini Vienna,Austria imesema Iran imeendelea kurutubisha madini ya Uranium na hivyo imekwenda kinyume na masharti ya Umoja wa Mataifa.Sasa Iran inakabiliwa na uwezekano wa kuwekewa vikwazo.Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa,John Bolton alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York alisema,Baraza la Usalama sasa linangojea kuona matokeo ya mkutano utakaofanywa Jumatano ijayo kati ya mkuu wa Umoja wa Ulaya kuhusu masuala ya kigeni,Javier Solana na mpatanishi mkuu wa Iran katika mgogoro huo wa kinuklia,Ali Larijani.Wakati huo huo waziri wa kigeni wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier amesema,bado ana matumaini kuwa kutapatikana suluhisho la kidplomasia.