1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoSenegal

Van Dijk: Jeraha la Mane ni pigo kwa Kombe la Dunia

18 Novemba 2022

Mchezaji nyota wa Senegal Sadio Mane ameondolewa kutoka kwenye kikosi cha timu yake ya taifa kitakachoshiriki mashindano ya Kombe la Dunia yanayoanza Jumapili huko Qatar.

https://p.dw.com/p/4JjM1
FC Bayern Muenchen vs. SV Werder Bremen, Sadio Mane
Picha: Sven Hoppe/picture alliance/dpa

Kulingana na Shirikisho la Kandanda la Senegal Mane aliyekuwa na jeraha la muundi hatokuwa imara kwa muda kuweza kushiriki mechi.

Baada ya tangazo hilo la Shirikisho la Kandanda la Senegal, klabu ya Mane Bayern Munich ilisema kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 na ambaye alichaguliwa katika nafasi ya pili kwenye tuzo za mchezaji bora duniani Ballon d'Or mwezi uliopita nyuma ya Karim Benzema, amefanyiwa upasuaji tayari huko Innsbruck na ataanza safari yake ya kuwa imara kurudi tena uwanjani kwa kufanya mazoezi madogo madogo mjini Munich katika siku chache zijazo.

Senegal haijataharuki na jeraha la mane

Alipata jeraha hilo la muundi alipokuwa akiichezea klabu yake ya Bayern mwezi huu ila alitajwa katika kikosi cha Kombe la Dunia cha timu yake kwa matumaini kwamba atakuwa imara kabla mechi ya kwanza ya timu yake.

Mkuu wa Shirikisho la Kandanda la Senegal Augustin Senghor ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba kikosi chao hakijawa na taharuki baada ya kumpoteza nyota huyo na kwamba afya ya mchezaji huyo ni muhimu na ndilo jambo lililowapelekea kufikia uamuzi huo.

Senegal watakuwa wanacheza mechi ya ufunguzi Jumatatu mwezi huu wa Novemba dhidi ya Uholanzi kwani wamepangwa katika Kundi A pamoja na wenyeji Qatar na Ecuador.

Nahodha wa timu ya taifa ya Uholanzi Virgil van Dijk amesema kukosekana kwa Mane ni pigo kwa kuwa Kombe la Dunia litakosa umahiri wake.

UEFA Nations League | Niederlande vs. Belgien | Virgil van Dijk, NIederlande
Nahodha wa Uholanzi Virgil van DijkPicha: Piroschka Van De Wouw/REUTERS

Van Dijk ambaye alikuwa mchezaji mwenza wa Mane katika klabu ya Liverpool kabla Msenegal huyo kuhamia Bayern, sasa atapambana na Senegal ambayo kwa kiasi fulani itakuwa hafifu katika mechi itakayochezwa uwanjani Al Thumama.

"Je, tunaisubiri kwa hamu mechi ya kwanza? Kwa kweli itakuwa mechi kubwa sana dhidi ya mabingwa wa Afrika na tutafanya kila tuwezalo ili tupate matokeo mazuri na tuanze kombe letu la dunia kwa mguu mzuri," alisema Van Dijk.

Mane anajiunga na orodha ndefu ya wachezaji nyota wenye majeraha

Mane lakini siye mchezaji nyota wa pekee aliyepata jeraha kabla ya mashindano haya.

FC Bayern Muenchen vs. SV Werder Bremen, Sadio Mane
Mane akifarijiwa na wachezaji wenzake baada ya kupata jeraha Picha: Sascha Walther/Eibner-Pressefoto/picture alliance

Ufaransa ambao ni mabingwa watetezi na mojawapo ya timu zinazopigiwa upatu kulinyakua kombe hilo, itazikosa huduma za Paul Pogba, Ngolo Kante, Christopher Nkunku, Presnel Kimpembe na Boubacar Kamara wote hao wakiwa walipata majeraha.

Ujerumani nayo itawakosa mshambuliaji wa RB Leipzig Timo Werner na nahodha wa Borussia Dortmund Marco Reus ambaye alipata jeraha siku chache kabla timu ya taifa kusafiri kuelekea Doha.

England pia imeathirika kiasi cha haja kwani watawakosa mabeki wa Chelsea Reece James na Ben Chilwell huku Ureno wakizikosa huduma za mshambuliaji wa Liverpool Diogo Jota na Pedro Neto wa Wolverhampton Wanderers.

Chanzo: Reuters/AFP