1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yavutana na Umoja wa ulaya juu kutekeleza matakwa yaliyowekwa

13 Aprili 2006

Uturuki haijakubali kufungua bandari zake wala viwanja vyake vya ndege kwa ajili ya shughuli za Cyprus.

https://p.dw.com/p/CBJ5
Kamishna wa Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso na waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Kamishna wa Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso na waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: AP

Uturuki imeingia kwenye hali ya mvutano na Umoja wa Ulaya juu ya kukataa kufungua bandari zake na viwanja vya ndege kwa shughuli za Cyprus.

Mvutano huu unatishia kuhatarisha suluhisho la Cyprus na mahusiano na Ugiriki.

Umoja wa Ulaya mwezi wa Oktoba unarajiwa kuchapisha ripoti ya maendeleo juu ya majadiliano ya kutaka kujiunga kwenye Umoja huo na serikali ya mjini Ankara.

Huenda ikapendekeza kuyafutilia mbali mazungumzo hayo ikiwa ni mwaka mmoja tangu yaanzishwe endapo Uturuki haitotekeleza matakwa ya umoja huo ya kutaka ifungue bandari zake pamoja na viwanja vya ndege.

Kwa mujibu wa wanadiplomasia na wadadisi wa mambo,ikiwa harakati za Uturuki za kutaka kujiunga kwenye Umoja wa Ulaya zitagonga mwamba basi itahatarisha kuimarika kwa mgawanyiko wa Cyprus na kuuzima uhusiano tete wa Uturuki na Ugiriki.

Cyprus iliyogawika tangu mwaka 1974 ilipovamiwa na Uturuki imeingilia juhudi zote zinazofadhiliwa na Umoja wa mataifa za kutaka kuziunganisha katika shirikisho na imekuwa kizingiti kikubwa kwa matumaini ya Uturuki ya kutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Cyprus ya Ugiriki inayoendesha serikali pekee inayotambulika kimataifa katika kisiwa cha Mediterranean iliupinga mpango wa amani wa Umoja wa mataifa katika kura ya maoni ya mwaka 2004 siku kadhaa kabla ya kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Lakini Cyprus ya Uturuki iliyotengwa na ambayo ni maskini iliupitisha.

Uturuki ilianzisha mazungumzo ya kutaka kujiunga na Umoja huo mwezi Oktoba uliopita na ili kufanikiwa kuifikia ndoto yake hiyo inabidi kutekeleza matakwa ya Umoja huo ambayo ni pamoja na kuzifungua bandari zake na viwanja vya ndege kwa shughuli za Cyprus lakini hadi sasa nchi hiyo imekataa katakata kufanya hivyo na badala yake wanataka masharti yalegezwe kwa Cyprus ya Uturuki.

Mehmet Ali Birand mwandishi wa maoni katika gazeti la kila siku la Uturuki la Posta anasema kutakuwepo na mgongano lakini Uturuki sio pekee ya kulaumiwa.

Ilipewa ahadi na Umoja wa Ulaya na serikali ya Uturuki haiwezi kubadili msimao kwa sababu ya maoni ya umma.

Rais wa Cyprus naye Tassos Papadopoulos ambaye serikali yake imetishia kutumia kura ya veto iwapo uturuki haitotekeleza matakwa yaliyowekwa anaonekana kutaka kuwa na usemi mkubwa.

Wadadisi hata hivyo wanasema baadhi ya wanachama ndani ya Umoja wa Ulaya hawapendelei kuliona taifa hilo lenye idadi kubwa ya waislamu likijiunga hivi karibuni na Umoja huo na huenda wakapigia upatu kucheleweshwa kwa mazungumzo hayo.