1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yasema Khashoggi alinyongwa na kukatwakatwa

Caro Robi
1 Novemba 2018

Mwendesha mashitaka Mkuu wa Uturuki Irfan Fidan amesema mwandishi habari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi aliuawa kwa kunyongwa punde tu alipoingia ubalozi mdogo wa Saudi Arabia wa Istanbul na kisha mwili wake ulikatwa.

https://p.dw.com/p/37VD3
Journalist Jamal Khashoggi
Picha: picture-alliance/AA/O. Shagaleh

Hayo yametangazwa muda mfupi tu baada ya mwendeshamashitaka mkuu wa Saudi Arabia Sheikh Saud al-Mojeb  kuondoka Uturuki na mwenzake wa Uturuki kusema alilazimika kufahamisha umma kuhusu mauaji ya Khashoggi baada ya mazungumzo kati yao kutozaa matunda.

al Mojeb aliyewasili Uturuki Jumapili iliyopita na kufanya mazungumzo na Fidan na maafisa wa shirika la ujasusi, aliondoka siku ya Jumatano bila ya kutoa taarifa yoyote.

Mwili wa Khasoggi uko wapi?

Mwili wa mwandishi huyo wa habari ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa mrithi wa kiti cha ufalme Mohamed Bin Salman haujapatikana mpaka sasa.

Mara ya mwisho kuonekana hai, ilikuwa tarehe 2 Oktoba alipokwenda katika ubalozi mdogo wa nchi yake mjini Istanbul kuchukua makaratasi ya mkuruhusu kufunga ndoa.

USA Washington Donald Trump zum Fall Khashoggi
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: picture-alliance/dpa/AP/E. Vucci

Rais wa Marekani Donald Trump amesema hahisi kusalitiwa na Saudi Arabia, na licha ya kuyaita mauaji hayo mabaya zaidi kuwahi kujaribu kufichwa, ameonya dhidi ya kusitisha uuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia akihoji itaathiri biashara za Marekani.

Hata hivyo waziri wa mambo ya nje Mike Pompeo amesema mauaji ya Khashoggi mwandishi wa habari wa gazeti la Marekani la Washington Post yanakiuka misingi ya sheria za kimataifa.

Msemaji wa chama tawala cha Uturuki Omer Celik amesema mauaji hayo hayangeweza kufanywa bila ya maagizo kutoka kwa maafisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Saudi Arabia.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amekuwa akitaka washukiwa wanaodaiwa kuhusika katika mauaji ya Khashoggi kurejeshwa Uturuki kufunguliwa mashitaka, jambo ambalo Saudi Arabia imekataa kufanya na pia kukataa kufichua mahali ulipo mwili wa Khashoggi.

Kwa upande wake, Ufaransa imesema juhudi za kutosha hazichukuliwi dhidi ya wauaji wa mwandishi huyo wa habari ambaye alikuwa mshirika wa karibu wa viongozi wa kifalme wa Saudia kabla ya kukimbilia Marekani mwaka jana.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/AP

Mhariri:Daniel Gakuba