1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAfghanistan

Uturuki yaitaka Afghanistan kutengua uamuzi wake

22 Desemba 2022

Uturuki imewatolea mwito watawala wa Taliban nchini Afghanistan kutengua uamuzi wao wa kuwazuia wanawake kujiunga na vyuo vikuu ikisema kitendo hicho sio cha kiislamu wala ubinadamu.

https://p.dw.com/p/4LJQL
Afghanistan -   Kunst by Künstlerin Sohiba Taraki
Picha: DW/AA

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu akizungumza mbele ya waandishi habari amesema hawakioni kuwa sawa kitendo hicho cha Taliban na kuhoji ni madhara gani ya kibinadamu yanayosababishwa na wanawake kupata elimu.

Marufuku hiyo ya utawala wa Taliban ambao uliahidi kulegeza sheria watakapoingia madarakani baada ya kumalizika vita vya miongo miwili, imekosolewa na viongozi mbalimbali duniani.

Marekani na Uingereza zimetowa matamshi makali ya kulaani uamuzi huo wa Taliban.

Utawala wa Taliban nchini Afghanistan mnamo siku ya Jumanne ulitangaza kuwazuia wanawake kote nchini humo kujiunga na vyuo vikuu, katika wakati ambapo serikali hiyo ya msimamo mkali wa Kiislamu ikiendelea kukiuka haki na uhuru wa wanawake wa kupata elimu. 

Licha ya kuahidi kulegeza misimamo yake wakati walipoingia madarakani mwezi Julai mwaka jana, Taliban imeendelea kuimarisha vizuizi katika kila eneo linalohusu maisha ya mwanamke wa Afghanistan, huku wakipuuzilia mbali ukosoaji wa kimataifa.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW