1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki na Urusi zakubaliana kusitisha mashambulizi Idlib

18 Septemba 2018

Marais wa Uturuki na Urusi wamekubaliana kuweka "eneo lisilokuwa na shughuli za kijeshi", katika mkoa wa Idlib nchini Syria, kwa lengo la kusitisha mashambulizi ya serikali ya Syria katika mkoa huo unaodhibitiwa na waasi

https://p.dw.com/p/353sW
Russland Sotschi Treffen Putin Erdogan
Picha: Reuters/A. Zemlianichenko

Makubaliano hayo yanaashiria ushindi wa kidiplomasia kwa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambaye alitaka kuepusha operesheni ya mashambulizi makali ya Syria, ikisaidiwa na ndege za kivita za Urusi, katika ngome ya mwisho iliyobaki ya waasi nchini Syria.

Akizungumza mwishoni mwa mkutano wake wa zaidi ya masaa matatu na Rais wa Uturuki Recep Erdogan mjini Sochi, Rais wa Urusi Vladmir Putin alisema wanamgambo wa itikadi kali watalazimika kujiondoa kutoka eneo hilo ambalo halitakuwa na shughuli za kijeshi. Eeneo hilo litakuwa na umbali wa kilomiota 15 hadi 20 kuingia ndani ya Idlib. Putin amesema wanajeshi wa Urusi na mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO – Uturuki watakuwa wakifanya doria zilizoratibiwa "Kama ilivyopendekezwa na rais wa Uturuki, ifikapo Oktoba 10, silaha zote nzito itabidi ziondolewe katika ukanda huu. vifaru na makombora ya kila aina ya makundi ya upinzani. mpango huu kwa jumla unaungwa mkono na serikali ya Syria. Katika siku chache zijazo, tutafanya mazungumzo ya ziada na uongozi wa Syria" Alisema Putin

Syrien Idlib Luftangriffe der Regierungskoaliltion
Idlib ndio ngome ya mwisho kuu ya waasi nchini SyriaPicha: Getty Images/AFP/O.H. Kadour

Mpango huo umeashiria makubaliano kati ya viongozi hao wawili na hivyo umechelewesha shambulizi la vikosi vya Syria na washirika wake Urusi na Iran, ambalo rais wa Uturuki Erdogan alihofia kuwa linaweza kusababisha mgogoro wa kibinaadamu karibu na mpaka wake. "Upinzani utabaki katika maeneo ambayo unayodhibiti kwa sasa. Kisha nasi tutahakikisha kuwa makundi ya itikadi kali hayaendeshi harakati zao katika ukanda huo salama. Urusi itachukua hatua zinazohitajika za dharura ili eneo hilo lisilo na shughuli za kijeshi la Idlib halishambuliwi". Amesema Erdogan

Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema juhudi za kidiplomasia kati ya Iran, Uturuki na Urusi zimefaulu katika kuepusha vita mkoani Idlib. 

Haijafahamika wazi ni vipi hasa mpango huo utakavyotekelezwa mkoani humo, ambako kuna Zaidi ya Wasyria milioni 3 na karibu wapiganaji waasi 60,000 kutoka makundi mbalimbali

Syrien Flüchtlinge Provinz Idlib
Wakaazi wa Idlib wakihamia maeneo salama kwa kuhofia mashambuliziPicha: Getty Images/AFP/A. Watad

Msemaji wa upinzani nchini Syria al-Aridi pamoja na Ahmed Ramadan, msemaji wa wapinzani wanaoishi uhamishoni wameyasifu makubaliano hayo. Ramadan amesema yameipa Urusi nafasi ya kuondokana na kitisho chake dhidi ya Idlib na ni mafanikio ya shinikizo la kidiplomasia kutoka kwa Uturuki na Marekani, ambayo pia ilipinga shambulizo hilo.

Naye Abu Omar, msemaji wa kundi la waasi wa Faylaq al-Sham lenye makao yake nchini Uturuki amempongeza Erdogan kwa kuzuia shambulizi na kuwapa waasi muda wa kuilinda ngome yao na watu wake. Msemai wa muungano wa wapiganaji wa upinzani unaofahamika kama National Front for Liberation ambao unaungwa mkono na Uturuki amesema juhudi za kidiplomasia zimeepusha mashambulizi ya Idlib lakini kundi lake linapaswa kufahamu kuhusu maelezo ya mpango huo na namna utakavyotekelezwa.

Kwingineko, ndege ya kivita ya Urusi iliyokuwa na wanajeshi 14 imetoweka kwenye mitambo ya kuongoza ndege ya radar katika bahari ya Mediterania jana usiku, wakati Syria iliposhambuliwa na makombora ya Israel.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema hatima ya wanajeshi wake bado haijulikani. Ndege hiyo ilikuwa ikirejea kwenye kituo cha kijeshi cha Hmeimim

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusra Buwayhid