1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki kwazidi kufukuta

4 Juni 2013

Jeshi la Polisi na waandamanaji wanaoipinga serikali nchini Uturuki wamekabiliana tena mjini Istanbul mapema Jumanne, huku kukiwa na taarifa kuwa idadi ya waliokufa katika vurugu hizo imefikia watu wawili.

https://p.dw.com/p/18jG9
Maandamano Uturuki yazidi kuwa makali
Maandamano Uturuki yazidi kuwa makaliPicha: Reuters

Mjini Istanbul Polisi ilitumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji waliochoma magari, kurusha mawe na kutoa miito kwa sauti za hasira mapema leo. Matukio kama hayo yalishuhudiwa pia mjini Ankara. Lakini waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan, ambae yuko ziarani nchini Morocco, amesisitiza kuwa hali imeanza kutulia.

Waziri mkuu wa Uturuki na manaibu wake, Bulent Arinc (Kushoto) na Beric Bozdag (kulia) akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Ataturk mjini Istanbul Jumatatu 03.06.2013 ambapo alitoa wito wa kuwepo na utulivu.
Waziri mkuu wa Uturuki na manaibu wake, Bulent Arinc (Kushoto) na Beric Bozdag (kulia) akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Ataturk mjini Istanbul Jumatatu 03.06.2013 ambapo alitoa wito wa kuwepo na utulivu.Picha: Reuters

"Matukio haya hayahusiki kwa namna yoyote ile na ukataji wa miti au ukarabati wa bustani.Wale walioshindwa katika uchaguzi ndio wako nyuma yake, maandamano hayafanyiki katika miji yote. Hali imetula sasa na watu wameanza kutumia akili zao. Kabla sijarudi nchini Uturuki, utulivu utakuwa umerejea" alisema Erdogan mjini Rabat, nchini Morocco.

Hakuna mapinduzi ya kiarabu Uturuki

Waziri mkuu Erdogan alikanusha madai ya mapinduzi kama yaliyotokea katika mataifa ya kiarabu na Waturuki, ambao wanamtuhumu kwa kujaribu kulaazimisha mageuzi yenye muelekeo wa Kiislamu katika taifa hilo lilsiloegemea dini. Maandamano hayo ambayo yameikumba miji kadhaa nchini Uturuki, yemeingia siku ya tano leo. Mjini Istanbul, Polisi ilikimbizana na maelfu ya waandamanaji waliokuwa wanataka kuisogelea ofisi ya waziri mkuu Erdogan, na uwanja wa mpira wa klabu ya Besiktas uliyopo karibu na ofisi hiyo.

Chama cha wahudumu wa afya kilisema siku ya Jumatatu mtu mmoja aliuawa baada ya gari kuwaparamia waandamanaji mjini Istanbul siku ya Jumapili. Na mapema leo, kituo binafsi cha Televisheni cha NTV kiliripoti kuwa kijana mwenye umri wa miaka 22 alifariki baada ya kupigwa risasi kichwani katika mkoa wa Hatay, kusini mwa nchi hiyo.

Waandamanaji wakitumia mwavuli mkubwa kujikinga wakati wa makabiliano na polisi wa kutulizaghasia mjini Istanbul.
Waandamanaji wakitumia mwavuli mkubwa kujikinga wakati wa makabiliano na polisi wa kutulizaghasia mjini Istanbul.Picha: Reuters

Makundi ya haki za binaadamu na madaktari wanasema zaidi ya watu 1000 wamejeruhiwa katika makabiliano mjini Istanbul, na 700 mjini Ankara. Serikali imesema raia 58 na maafisa usalama 115 wamejeruhiwa, na kwamba vurugu zimeripotiwa katika miji 67. Serikali pia ilisema watu 1,700 wamekamatwa nchini kote.

Rais Gul awatuliza waandamanaji

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amezitaka pande kuepuka kuchochea vurugu. Mshirika wa waziri mkuu Erdogan, rais Abdullah Gul ametoa wito wa kuwepo na utulivu, na kuwahakikishia waandamanaji kuwa sauti zao zitasikilizwa. "Kama kuna mapingamizi au ukosoaji ukiacha wakati wa uchaguzi, ni jambo la kawaida kwa watu kuonyesha hisia zao. Nataka watu wajue kwamba ujumbe muhimu kutoka kwa waandamanji hao umefika," alisema Gul baada ya kukutana na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Kilicdaroglu.

Machafuko hayo yamedhihirisha wasiwasi unaoikumba Uturuki, ambayo licha ya kuwa taifa lisiloegemea dini kwa mujibu wa katiba yake, wakaazi wake wengi ni Waislamu. Soko la hisa la Istanbul lilishuka thamani siku ya Jumatatu kwa asilimia 10 na sarafu ya Uturuki Lira ilishuka dhidi ya euro na dola. Chama cha wafanyakazi wa umma KESK, kimeitisha mgomo wa siku mbili kupinga ukandamizaji wa waandamanaji.

Polisi wa kutuliza ghasia akifyatua gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji mjini Ankara.
Polisi wa kutuliza ghasia akifyatua gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji mjini Ankara.Picha: Reuters

Demokrasia katika sanduku la kura

Wimbi la maandamano hayo lilianza baada ya polisi kukandamiza kile waandamanaji wanachosema yalikuwa maandamano ya amani mjini Istanbul, dhidi ya mipango ya kujenga juu ya bustani ya Gez, eneo la kijani lililo karibu na uwanja wa Taksim. Hatua hiyo ilichochea maandamano zaidi mjini Istanbul, Ankara na katika miji kadhaa mingine.

Erdogan amekuwa akisisitiza kuwa demokrasia inatokana na sanduku la kupigia kura, na kuwataka wale wasiopendezwa na sera zake wasubiri wakati wa uchaguzi. Uturuki itafanya uchaguzi mwakani, na waangalizi wanatarajia kuwa waziri mkuu huyo atagombea urais.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Daniel Gakuba