1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki kuwashambulia waasi wa Kikurdi nchini Syria

Sylvia Mwehozi
13 Desemba 2018

Uturuki imesema itafanya operesheni mpya ya mashambulizi nchini Syria dhidi ya kundi la wanamgambo wa Kikurdi linaloungwa mkono na Marekani, lakini Uturuki yenyewe inalichukulia kuwa kundi la kigaidi.

https://p.dw.com/p/3A0dr
Syrien türkische Soldaten in Afrin
Picha: Getty Images/AFP/O.H. Kadour

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan alisema katika hotuba yake mjini Ankara kwamba wataanza operesheni hiyo katika siku chache zijazo, kulikomboa eneo linaloshikiliwa na kundi la Kikurdi la YPG.

"Tumesema na tunasema tena sasa kwamba tutaanzisha operesheni ya kulikomboa eneo la mashariki mwa mto Euphrates kutoka kundi linalotaka kujitenga katika siku chache zijazo. Lengo letu si askari wa Marekani, bali kundi la kigaidi ambalo linafanya kazi zake katika mkoa huo," amesema Erdogan.

Uturuki inasema kundi la YPG ni tawi la chama cha wafanyakazi cha Wakurdi PKK ambalo lilipigwa marufuku na limekuwa na upinzani dhidi ya taifa la Uturuki tangu mwaka 1984. PKK imeorodheshwa kama kundi la kigaidi na Uturuki pamoja na washirika wake wa nchi za magharibi.

Vikosi vya Marekani vinafanya kazi kwa karibu na YPG chini ya muungano wa majeshi ya Kikurdi yanayoongozwa na jeshi huru la Syria SDF dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS. Uhusiano wa Marekani na kundi la YPG, kama mshirika muhimu ni moja ya chanzo kikuu cha mvutano baina ya Uturuki na Marekani. Uturuki imerejelea kuituhumu Marekani kwa kuwapatia misaada ya kijeshi wanamgambo wa Kikurdi.

Deutschland Türkischer Präsident Erdogan in Köln
Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan Picha: Reuters/W. Rattay

Hata hivyo wanamgambo wa kikurdi wakiungwa mkono na Marekani nchini Syria, wameonya kwamba shambulizi lolote litakalofanywa na Uturuki dhidi yao, litakwamisha mapambano dhidi ya kundi la IS. Jeshi la SDF lilifanya mashambulizi mwezi Septemba kuwaondoa IS mashariki mwa mto Euphrates karibu na mpaka na Iraq.

Uturuki ina hofu kwamba kuendelea kupanuka kwa kundi la kikurdi karibu na mpaka kutachochea shauku ya kujitenga ndani ya nchi yake. Mwezi Januari, vikosi vya Uturuki viliwaunga mkono waasi wa Syria kuliondoa kundi la YPG kutoka ngome ya kaskazini magharibi mwa Afrin, magharibi mwa mto Euphrates.

Nayo wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon imesema hatua yoyote ya kijeshi katika eneo la kaskazini mwa Syria "haikubaliki". Pentagon mara kwa mara imeonya kwamba mapigano yoyote baina ya Uturuki na SDF ni kuvuruga lengo kuu la Marekani la kupambana na IS nchini Syria.

Msemaji wa Pentagon Kamanda Sean Robertoson ameeleza kwamba hatua yoyote ya kijeshi kaskazini mashariki mwa Syria itakuwa ni "wasiwasi mkubwa" kwa sababu itahatarisha vikosi vya Marekani vinavyofanya kazi na majeshi ya SDF katika mkoa huo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Josephat Charo