1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki inaamua kati ya Erdogan au Kiliçdaroglu

28 Mei 2023

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa asubuhi ya leo kote nchini Uturuki kwa duru ya pili ya uchaguzi wa rais itakayoamua mwanasiasa atayeliongoza kwa miaka mitano taifa hilo la pili kwa idadi kubwa ya watu barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/4Rue0
Türkei | Präsidentschaftswahl | Erste Stichwahl
Picha: Yves Herman/REUTERS

Karibu wapiga kura milioni 61 wanashiriki uchaguzi huo unaofanyika kuanzia saa mbili asubuhi hadi majira ya saa kumi na moja jioni kwa saa za Uturuki.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya duru ya kwanza kushindwa kutoa mshindi wa wazi kati ya rais aliye madarakani anayewania muhula mwingine Recep Tayyip Erdogan dhidi ya mpinzani wake mkuu Kemal Kiliçdaroglu. 

Soma zaidi: Uchaguzi wa Uturuki na athari zake katika uhusiano na Afrika

Kura ya leo inatajwa kuwa kipimo cha utawala wa miongo miwili ya Erdogan anayetuhumiwa na upinzani kwa sera za "mabavu".

Uchaguzi huo unafanyika Uturuki ikiwa imepita miezi mitatu tangu kutokea tetemeko kubwa la ardhi lililowaua maelfu ya watu na katikati ya mdodoro mkubwa wa kiuchumi kuwahi kushuhudiwa.

Mfahamu Recep Tayyip Erdogan anayetetea kiti chake

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameitawala nchi hiyo kwa takriban miaka 20 licha ya mihula yake kugubikwa na masaibu chungu nzima ikiwemo migorogoro ya kisiasa, maaandamano makubwa, kashfa za rushwa ,jaribio la mapinduzi ya kijeshi na hata wimbi kubwa la wakimbizi wanaokimbia vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Hata baada ya miaka 20 ya utawala wenye misukosuko mingi rais Erdogan inaonesha bado ni mtu mashuhuri nchini Uturuki.  Hivi sasa raia wa Uturuki wanakabiliwa na mfumuko mkubwa wa bei na wengi wao bado wana hali ngumu ya maisha tangu kutokea tetemeko la ardhi mnamo mwezi Februari mwaka huu. Baadhi ya raia nchini Uturuki  wanaelezea kuwa hali hiyo mbaya imechagizwa na mwitikio wa mwendo wa kinyonga wa serikali ya Erdogan.

Rais Recep Tayyip Erdogan na mkewe Emine Erdogan wakipiga kura
Rais Recep Tayyip Erdogan na mkewe Emine Erdogan wakipiga kuraPicha: Murad Sezer/AP Photo/picture alliance

Hata hivyo kiongozi huyo anaetajwa kuwa na chembe za utawala wa kimabavu anaingia katika duru ya pili ya uchaguzi siku ya Jumapili kukabiliana na mpinzani wake Kemal  Kilicdaroglu mara baada ya kushindwa kufikisha zaidi ya asilimia 50 ya kura zote katika duru ya kwanza ya uchaguzi.

Rais Recep Tayyip Erdogan mwenye umri wa miaka 69 anatajwa kukubalika na wafuasi wa kihifadhina na viongozi wakuu wa dini ya kiislam katikia nchi ambayo kwa miongo mingi imekuwa inatajwa kutokuwa na misingi ya dini.

Erdogan alivyofanikiwa kudumisha umashuhuri wake mbele ya waturuki

 Kiongozi huyo ameimarisha mbawa zake za kisiasa kwa kuboresha miundombinu ili kujiongezea tiketi ya uungaji mkono kutoka kwa wapiga kura ingawa kwa upande mwingine amethibiti uhuru wa vyombo va habari kwa lengo la kuwanyamazisha  wakosoaji wake.

Wafuasi wake wanavutiwa na namna kiongozi huyo anavyoshughulikia masuala ya kimataifa na wameaminishwa kwamba nchi yao inaweza kujitegemea bila kuchukua upande wa nchi za magharibi ama mashariki na pia jeshi lao lina uwezo wa kukabiliana na yeyote kwa namna yao na wala sio kutokana na maoni ya wachambuzi wa kimataifa.

Gonul Tol mchambuzi katika Taasisi ya masuala ya Mashariki ya Kati huko Washington alinukuliwa akisema kuwa wapiga kura nchini Uturuki hawana imani na upinzani kubadilisha mambo nchini humo. Anasema katika nyakati za changamoto nyingi kama ilivyo sasa wananachi hupenda kuwa nyuma ya kiongozi ambaye tayari ameonesha mfano.

Mpinzani wake mkuu, Kemal Kilicdaroglu, ambaye ni mwanauchumi na mbunge wa zamani ameahidi kutengua sera za kiuchumi za Erdogan ambazo wataalamu wanasema kuwa zimechochea mfumuko wa bei na kubadili mwelekeo wa kisiasa nchini humo huku akituhumu utawala wa kimabavu wa Erdogan ikiwa ni pamoja na kukandamiza uhuru wa kujieleza. Sera ambazo wafuasi wa Erdogan wamezitupilia mbali.

Mpinzani mkuu wa Erdogan, Kemal Kilicdaroglu
Mpinzani mkuu wa Erdogan, Kemal KilicdarogluPicha: Yves Herman/REUTERS

Baadhi ya wafuasi wa Erdogan wanaeleza kwamba hakuna rais kama Erdogan duniani kote na nchi yao imepiga hatua kubwa kwa kipindi cha miaka 20 ya kiongozi huyo na wanahofu kuwa huenda mambo yakarudi nyuma kwa miaka mingine 50 ama 60 kama upinzani utaingia madarakani.

Uturuki ambayo ni mwanachama muhimu wa NATO kwa sababu ya eneo lake la kimkakati kwenye njia panda ya Ulaya na Asia inadhibiti jeshi kubwa la pili katika muungano huo, na chini ya utawala wa Erdogan, Uturuki imejidhihirisha kuwa mshirika muhimu na wakati mwingine msumbufu kwa NATO. Imewahi kupinga kuingizwa kwa Sweden katika umoja huo huku ikinunua Mfumo wa kujilinda na makombora kutoka Urusi kitendo ambacho kiliilazimisha Marekani kuiondoa uturuki katika mradi wake wa kuunda ndege za kisasa za kivita.

Baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe kuzuka nchini Syria mwaka 2011 Erdogan aliwaunga mkono wapiganaji wa upinzani wanaotaka kumuondoa rais Bashar Al Assad na amekuwa akifanya hivo kama njia ya kukabiliana na mataifa ya magharibi kwa kutishia kufungua mipaka na kwa sasa jeshi la Uturuki linadhibiti eneo kubwa la kaskazini mwa Syria, masuala ambayo yanatafsiriwa kuwa ujeuri wa Erdogan kwa mataifa ya maharibi.

Erdogan anajigamba kuimarisha sekta yake ya kijeshi na viwanda na sasa yupo kwenye kampeni  ambayo amezitaja kuwa ya ndege zisizo na rubani, Meli ya kivita za kisasa inayotajwa kuwa ya kwanza duniani na pia ameondoa sheria kali za jeshi zilizokuwa zinazuia uvaaji wa hijab shuleni na ofisini.

Changamoto zinazomkabili Erdogan

Changamoto kubwa kwa Erdogan kwa sasa ni uchumi, mfumuko wa bei ni moja ya changamoto kubwa licha yab kufanyika jitihada kadhaa za serikali yake ikiwa ni  kuongeza mishahara kwa wafanyakazi wa umma na kufuta madeni katika kaya maskini.

Sehemu ya athari za tetemeko la ardhi la Februari 21, 2023 Uturuki
Sehemu ya athari za tetemeko la ardhi la Februari 21, 2023 UturukiPicha: CLODAGH KILCOYNE/REUTERS

Erdogan ameahidi kujenga upya maeneo makubwa yaliyoathirika na tetemeko liloua zaidi ya watu 50,000 nchini uturuki na katika duru ya kwanza ya uchaguzi alishinda katika majimbo 10 kati ya 11 yaliyoathirika na tetemeko hilo na wafuasi wake katika maeneo hayo wanamuunga mkono na wanadai kuwa ni kweli kwamba kuna changamoto za kupanda kwa gharama za maisha lakini  ni changamoto ya dunia nzima na sio uturuki pekee.

Wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi uliofanyika Mei 14, Uturuki ilifanya pia uchaguzi wa wabunge ambapo muungano wa Erdogan wa vyama vya kitaifa ulipata wingi wa kura katika bunge kwa kushinda viti 600 hatua ambayo inampa faida kiongozi huyo katika duru hii ya pili ya uchaguzi