1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki imeikosoa Marekani kwa kuiwekea vikwazo

Yusra Buwayhid
15 Desemba 2020

Uturuki imeikosoa Marekani kwa kuiwekea vikwazo, baada ya kununua mfumo wa ulinzi wa anga kutoka Urusi wa S-400. Lakini imesema hilo halitoharibu uhusiano wao kama washirika wa jumuiya ya kujihami NATO.

https://p.dw.com/p/3ml3a
Russland S-400 Raketenabwehr an Grenze zur Türkei
Picha: Reuters/Ministry of Defence of the Russian Federation

 

Ismail Demir, mkuu wa shirika la ununuzi wa silaha Uturuki amesema uhusiano wa nchi hizo mbili hautaathiriwa licha ya uamuzi wa utawala wa Rais Donald Trump hatimaye kuiadhibu Uturuki kwa kununua mfumo wa ulinzi wa anga kutoka Urusi.

Amesisitiza kwamba Marekani na Uturuki ni washirika wa Jumuiya ya kujihami NATO, na wataendelea kufanya kazi pamoja. Lakini pia amesema vikwazo hivyo vitaangaliwa kama onyo na Uturuki, na kuvihamasisha viwanda vyake vya kutengeneza vifaa vya ulinzi kuharakisha kazi zao.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan amesema kuiweka vikwazo nchi yake ni kuikosea heshima. Aidha Erdogan amesema amesikitishwa sana na hali iliyojitokeza.

"Inasikitisha kwamba maneno ya kuiwekea vikwazo nchi yetu yameongezeka kutoka Umoja wa Ulaya na michakato ya kufanya hivyo imeshaanzishwa na Marekani. Kwa kweli, tunatarajia Umoja wa Ulaya hautoidhinisha vikwazo, lakini badala yake utatimiza ahadi yake iliyoshindwa kuitimiza kwa miaka ya kutupa uanachama kamili," amesema Erdogan.

Iran yaitetea Uturuki

Waziri wa Mambo ya nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif, Jumanne ameilaani Marekani kwa kuiwekewa vikwazo nchi jirani ya Uturuki. Kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter Zarif, amesema kwa kufanya hivyo Marekani imedhihirisha kuwa haiheshimu sheria za kimataifa.

Türkei, Ankara: Recep Tayyip Erdogan und Wladimir Putin schütteln sich die Hände
Rais wa Urusi Vladimir Putin akiwa na wa Uturuki Reccep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/abaca/Depo Photo

Mkurugenzi wa mawasiliano wa Uturuki, Fahrettin Altun, ameandika Twitter kwamba uhusiano kati ya Marekani na Uturuki ni muhimu sana, na matarajio yake ni kwamba Marekani itabatilisha uamuzi wake huo.

Vikwazo hivyo vilivyotangazwa jana Jumatatu ni sehemu ya sheria ya Marekani iitwayo CAATSA, inayolenga kupunguza ushawishi wa Urusi ulimwenguni.

Vikwazo hivyo vimemlenga Demir na maafisa wenzake watatu. Na kuanzia sasa mali zozote wanazozimiliki Marekani zitakamatwa na pia watazuiliwa kuingia nchini humo. Aidha leseni kadhaa za kununulia silaha pamoja na mikopo vimepigwa marufuku kwa shirika hilo la kununua silaha la Uturuki.

Ni mara ya kwanza kwa Marekani kuitumia sheria hiyo ya CAATSA dhidi ya mshirika wa NATO.

Uturuki ilinunua mfumo huo wa ulinzi wa kutumia makombora ya anga mnamo mwaka 2019, na kuujaribu kwa mara ya kwanza Oktoba mwaka huu.

Vyanzo: (ap,rtre)