1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utekaji nyara watoto watumika kama mbinu ya vita Msumbiji

9 Juni 2021

Wanambambo wa itikadi kali ambao wamekuwa wakiendesha harakati zao kaskazini mwa Msumbuji waliwateka nyara watoto wakati wa uvamizi wao wa mwaka wa 2020

https://p.dw.com/p/3uc2u
Ntele Montepuez Neuansiedlung
Picha: DW

Mashirika ya misaada yamesema makundi yenye silaha nchini Msumbiji yanaendelea kuwateka nyara watoto kama mbinu ya kutumika vitani, hatua inayowaweka waathiriwa katika hatari ya kunyanyaswa kingono, ndoa za mapema na kutumiwa kama wapiganaji katika mgogoro unaoendelea kuwa mbaya nchini humo. 

Karibu watoto 51 wametekwa nyara kwa mwaka mmoja uliopita katika machafuko ambayo yamewauwa maelfu ya watu na kuwaacha wengine bila makaazi katika eneo la kaskazini lililoharibiwa na uasi wa itikadi kali, lakini wafanyakazi wa misaada wanasema idadi ya matukio ya utekaji nyara huenda iko juu mno. Mkurugenzi wa Shirika la Save The Children tawi la Msumbuji Chance Briggs anasema utekaji nyara wa mtoto ni moja kati ya matukio sita makubwa ya ukiukaji dhidi ya watoto katika nyakati za migogoro kama inavyoelezwa na Umoja wa Mataifa. Nura ni mama mwenye umri wa miaka 42 ambaye binti yake alitekwa nyara "Waliwachukua binti zetu na kuwafungia katika nyumba tofauti. Na wakatuchukua na kutunfungia katika nyumba nyingine. Baadaye wakarudi na kuwachukua wasichana waliowavutia. Waliwaacha wanawake ndani ya nyumba. Jioni, baada ya kuwachukua binti zetu, tukafanikiwa kutoka."

Ntele Montepuez Dorf
Zaidi ya watu 700,000 wameachwa bila makaaziPicha: DW

Ukosefu wa usalama unaohusishwa na uasiambao ulizuka katika nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika mwaka wa 2017 umesababisha watu Zaidi ya 700,000 kukimbia makazi yao, huku karibu nusu ya waliopoteza makazi ikikadiriwa kuwa Watoto wadogo. Paula Sengo, mshauri wa ulinzi wa Watoto katika shirika la Save The Children nchini Msumbuji anasema hali ni ya kutia wasiwasi. "Kwa sasa, visa vilivyoripotiwa vya ukiukaji wa haki za watoto vinaongezeka sana. Sasa tumeona visa vya unyanyasaji wa kingono."

Soma pia: Wakuu wa SADC walaani uasi nchini Msumbiji

Waathiriwa wa utekaji nyara aghalabu hukumbwa na kiwewe kama vile kushuhudia watu kukatwa vichwa au kuziona nyumba zao zikichomwa moto.

Wako kwenye hatari kubwa

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu linasema limeorodhesha Zaidi ya maombi 2,600 nchini Msumbuji kati ya Septemba 2020 na Aprili 2021 kutoka kwa watu waliowapoteza jamaa zao, wengi wao wakiwa vijana na Watoto. James Mathews, naibu mkuu wa shirika hilo mjini Maputo anasema kuna idadi kubwa mno ya Watoto wasioongozana na mtu ambao wako katika hatari kubwa ya kukumbwa na kila aina ya ukiukaji na unyanyasaji.

Soma pia: EU huenda ikatuma ujumbe wa kijeshi Msumbiji katika miezi ijayo

Watoto hawatumikishwi tu jeshini na makundi mengine kama wapiganaji. Pia wanatumiwa kama watoa habari, waporaji, wajumbe, wapelelezi au kama watumwa wa majumbani au wa ngono

Mohamed Malick Fall, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto – UNICEF kanda ya mashariki na Kusini mwa Afrika anasema hali ya watoto katika mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado inaanza kuwa tete mno.

Reuters