1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamlaka ya Nagorno Karabakh yafutwa

28 Septemba 2023

Uongozi wa Jamhuri ya jimbo la Nagorno Karabakh wakubali kufuta mamlaka yake na kutangaza kuachia ngazi Januari mosi 2024,hatua inayofikisha mwisho kelele za kujitenga

https://p.dw.com/p/4WuAI
Flucht aus Bergkarabach
Picha: Gaiane Yenokian/AP Photo/picture alliance

Mpaka hivi sasa maelfu ya watu wa Nagorno Karabakh wameshakimbilia Armenia na wataalamu wanasema wanatarajia kimsingi Jamii nzima ya Warmenia wanaoishi kwenye jimbo hilo wataondoka.

Na taarifa zilizochapishwa leo na vyombo vya habari zinasema kwamba wale waliojitangaza kuwa Jamhuri ya Artsakh ambao ndio watawala wa eneo hilo lenye mzozo la Nagorno Karabakh wamekubalia kuachia ngazi na kuwa tayari kuifuta jamhuri hiyo kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2024.

Hatua hiyo inakuja baada ya rais Samvel Shahramanyan anayeliongoza jimbo hilo kusaini amri ya kufuta uwepo wa jamhuri hiyo ya Nagorno Karabakh kuanzia mwaka 2024,na utekelezwaji wa amri hiyo umeanza leo asubuhi.

Vyombo vya habari wa nchini Armenia vimeripoti kwamba Jamhuri ya Artsakh ambayo pia inajulikana kama Jamhuri ya Nagorno Karabakh imeamuwa kufuta mamlaka yake yote kufikia tarehe 1 Januari mwaka ujao baada ya kushindwa kwa vikosi vyake katika operesheni kubwa iliyoendeshwa na jeshi la Azerbaijan hivi karibuni.

Amri hiyo imefafanua kwamba uamuzi huo umechukuliwa kwasababu ya hali ya kisiasa na kijeshi ya hivi sasa na inalenga hasa kulinda usalama na maisha ya wakaazi katika jimbo hilo.Lakini pia kwa upande mwingine mahakama ya Azerbaijan imemuweka kizuizini aliyekuwa kiongozi wa wanaopigania kujitenga Ruben Vardanyan kusubiri kuendeshwa kwa kesi dhidi yake baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kufadhili ugaidi na matukio mengine ya uhalifu.

Ruben Vardanyan,kiongozi wa zamani wa wanaopigania kujitenga jimbo la Nagorno Karabakh
Kiongozi wa zamani wa wanaotaka kujitenga,Nagorno Karabakh-Ruben Vardanya,akishikiliwa na polisi wa AzerbaijanPicha: State Security Service of Azerbaijan/Handout/REUTERS

Wakati hayo yakijitokeza,rais wa Azerbaijan kwa upande mwingine amefanya ziara kwenye jimbo hilo la Nagorno Karabakh hii leo akiutembelea mji wa Jabrayil kukagua miradi ya ujenzi kwenye eneo hilo,ikiwa ni hatua iliyokuja siku chacha  baada ya wanajeshi wake kulidhibiti tena eneo hilo.

Rais t Ilham Alijev wa Azerbaijan
Rais t Ilham Alijev wa Azerbaijan akilihutubia taifa septemba 20.mwaka 2023Picha: Press Service of the President of Azerbaijan Ilham Alijew/REUTERS

Japo haikuwekwa wazi ziara hiyo imefanyika wakati gani lakini inaonesha ni mara ya  kwanza ya rais huyo kuitembelea Nagorno Karabakh tangu operesheni ya kijeshi. Mji huo wa Jabrayil ulitekwa na vikosi vya wenye asili ya Armenia Waliopigania kujitenga kwa jimbo hilo katika miaka ya 1990 baada ya kuvunjika kwa muungano wa Soviet na ukarudi mikononi mwa Azerbaijan kufuatia vita vya muda mfupi vya mwaka 2020.

Historia

Katika historia fupi ni kwamba  jimbo la Nagorno Karabakh linazozaniwa kwa miongo kadhaa kati ya nchi hiyo ya Azerbaijan na Armenia ambao ni majirani na wote walikuwa chini ya muungano wa Kisovieti kabla ya kuvunjika kwake.

Na katika miaka ya 1990 jimbo hilo ambalo kimsingi limo ndani ya Azerbaijan na linatambuliwa kimataifa kama milki ya Azerbaijan lilifanikiwa kujitenga na nchi hiyo katika vita vikubwa vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha umwagaji mkubwa wa damu  likisaidiwa na Armenia.

Maelfu ya Warmenia wa Nagorno Karabakh wakikimbilia Armenia
Maelfu ya Warmenia wa Nagorno Karabakh wakilikimbia jimbo hiloPicha: Alexander Patrin/TASS/dpa/picture alliance

Na kisha viongozi wa jimbo hilo wakatangaza kuunda jamhuri yao ya Arsakh ambayo kwahakika haitambuliwi.Wengi wa wakaazi wa jimbo hilo ni wenye asili ya Armenia na kufikia leo Alhamisi utawala wa Armenia umefahamisha kwamba wakaazi 65,000 kutoka jimbo hilo wameingia Armenia.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW