1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utafiti: Vyuo vikuu Ulaya vyashirikiana na China

19 Mei 2022

Imegundulika kuwa vyuo vikuu na watafiti kadha barani Ulaya wanashirikiana na taasisi za kijeshi za China kwa mujibu wa ugunduzi wa kimataifa uliopewa jina la "Uchunguzi wa Sayansi ya China".

https://p.dw.com/p/4BYBL
SPERRFRIST | Banner Projekt C | China Science Investigation

"Uchunguzi wa Sayansi ya China" uliofanywa na mashirika ya Correctiv, Follow the Money kwa kushirikiana na Deutschlandfunk, Süddeutsche Zeitung, Deutsche Welle na vyombo vyengine vya habari vya Ulaya umegunduwa kuwa katika takribani matukio 3,000, watafiti hapa barani Ulaya wamewahi kushirikiana na wenzao kutoka vyuo vikuu vya kijeshi vya China katika miradi ya tafiti za kisayansi za masuala ya kiraia, lakini ambazo matokeo yake yanaweza pia kutumika kwa malengo ya kijeshi. 

Utafiti huo pia umegunduwa kwa uchache machapisho 349 ya kitaalamu yakiwahusisha Wajerumani. Vile vile, watafiti kutoka angalau vyuo vikuu 48 vya Ujerumani wanashirikiana na taasisi ya taaluma nchini China ambayo ina ukaribu mkubwa na jeshi.

"Kwa asilimia 100, Ujerumani ina wasiwasi sana linapokuja suala la ushirikiano wa kisayansi na China," alisema mtaalamu mashuhuri wa masuala ya China, Didi Kirsten Tatlow, akiongeza kuwa "utawala wa kikomunisti unajaribu kupata maarifa ya kimkakati na nguvu kupitia ushirikiano huu wa tafiti."

Khofu ya vyombo vya usalama

Rubaa za kiusalama nchini Ujerumani zinavionya na kuvituhumu vyuo vikuu kwa kuichukulia China kuwa mshirika.

China Genmanipulation DNA gene-editing
Mfanyakazi wa afya nchini China akipima mayai yaliyopandishwa kwa ajili ya watoto wanaozaliwa maabara.Picha: Wei Liang/dpa/HPIC/picture alliance

Kwa mujibu wa wataalamu hao wa masuala ya usalama, uongozi wa kikomunisti wa China unahitaji sana kupata maarifa kwenye maeneo kama vile teknolojia ya habari, anga, kilimo na akili ya kutengeneza.

Juu ya yote, uchunguzi huo uliofanywa kwa ushirikiano wa mashirika mawili ya utafiti ya Correctiv na Follow the Money kwa ushirikiano wa vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo Deutsche Welle, umebaini kwamba mabadilishano ya kisayansi na Chuo Kikuu cha Taifa cha Teknolojia ya Ulinzi cha China yana matatizo, kwa sababu chuo hicho kinawajibika moja kwa moja Kamisheni Kuu ya Kijeshi, chombo cha juu kabisa cha kijeshi kwenye Jamhuri ya Watu wa China.

Vyuo vikuu vya Bonn, Hamburg vyaongoza kwenye ushirikiano na China

SPERRFRIST Projekt C | Präsident Xi Jinping, Besuch in Zhuhai
Rais Xi Jinping akizungumza na wataalamu wa utafiti wa teknolojia ya matibabu.Picha: Xie Huanchi/Xinhua News Agency/picture alliance

Utafiti huo unaonesha kwamba, tangu mwaka 2000, angalau machapicho 230 yameandikwa kwa ushirikiano kati ya watafiti wa Ujerumani na Chuo Kikuu hicho. Kinara kwenye orodha ni Chuo Kikuu cha Hamburg kikifuatiwa na Taasisi ya Max Planck, Chuo Kikuu cha Magdeburg na Chuo Kikuu cha Bonn.

Kwa mfano, machapisho mawili yalishughulika na kuwafuatilia watu ama kuimarisha uwezo wa maroboti kufuatilia, maarifa yanayoweza kutumika sio tu kwenye eneo la kiraia bali pia la kijeshi.

Hata hivyo, taasisi wa utafiti zilizowasiliana na watafiti hawa zinaliona jambo hili tafauti.

Serikali kuu ya shirikisho inafahamu juu ya tatizo lenyewe, lakini nayo pia haiwezi kufanya kazi bila ya kushirikiana na China kabisa kabisa, kama vile kwenye tafiti kuhusu masuala ya bahari na mabadiliko ya tabianchi.

"Mwamko kwa kweli ni wa juu sana na ni muhimu kutafuta uwiano mzuri. Kwa maneno mengine, shirikianeni pale ambapo kweli kuna maslahi ya Ujerumani na Ulaya. Lakini mashirikiano ambayo yanapelekea kwenye kusaidia utafiti wa kijeshi wa China, hayaingii kwenye mashirikiano yanayofaa," anasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Utafiti, Jens Brandenburg.