1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishwaji mapigano kuanza Gaza, mateka kuachiwa

24 Novemba 2023

Israel na kundi la Hamas wataanza kuutekeleza asubuhi hii mpango wa kusitisha mapigano kwa muda wa siku nne, huku kundi la kwanza la mateka 13 wanaoshikiliwa Gaza ambao ni wanawake na watoto wakiachiwa huru baadae leo

https://p.dw.com/p/4ZNwo
Operesheni ya ardhini ya Israel dhidi ya Hamas kaskazini mwa Gaza
Qatar imesema mpango huo utajumuisha usitishwaji mpana wa vita kaskazini na kusini mwa GazaPicha: Ronen Zvulun/Reuters

Madola ya ulimwengu yamezipokea habari hizo kwa tahadhari. Lakini mapigano yalipamba moto wakati muda ukikaribia wa kuanza kutekelezwa makubaliano hayo ya kusitisha vita vilivyodumu kwa karibu wiki saba. Pande zote pia zimeashiria kuwa mpango huo utakuwa wa muda na ziko tayari kuendelea na operesheni zao baadae.

Soma pia: Qatar imesema usitishaji mapigano utaanza kutekelezwa Ijumaa asubuhi na kufuatiwa na kuachiliwa kwa mateka 13 alasiri

Wizara ya mambo ya kigeni ya Qatar imesema usitishwaji mapigano utaanza saa moja kamili asubuhi saa za Gaza na utahusisha usitishwaji mpana wa vita kaskazini na kusini mwa Gaza. Msaada wa ziada utaanza kuingia Gaza na mateka wa kwanza wakiwemo wanawake wazee wataachiwa huru saa kumi kamili jioni. Idadi ya jumla itaongezeka hadi 50 kwa kipindi cha siku nne. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar Majed al-Ansari hata hivyo hakusema ni wafungwa wangapi wa Kipalestina watakaoachiwa, lakini maafisa wamesema watatu wataachiwa kwa kila mateka mmoja. Hamas imethibitisha kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram kuwa uhasama wote kutoka kwa wanajeshi wake utasitishwa.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar Majed Al-Ansari mjini Doha
Qatar ni mpatanishi wa mzozo wa Israel na HamasPicha: Imad Creidi/REUTERS

Israel imeithibisha orodha ya mateka

Jeshi la Israel lilisema askari wake watabaki nyuma ya sehemu zitakazositisha vita ndani ya Gaza. Msemaji wa jeshi Daniel Hagari amesema hizi zitakuwa nyakati ngumu na hakuna chenye uhakika kwa sababu hata wakati wa mchakato huu kunaweza kutokea mabadiliko.

Soma pia: Qatar imesimama kama mpatanishi mkuu katika mazungumzo ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza

Israel imethibitisha kuwa imepokea orodha ya mwanzo ya mateka watakaoachiwa kutoka Gaza, kwa mujibu wa shirika la Habari la Reuters.

Taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imesema maafisa husika wanathibitisha maelezo ya majina hayo na wanawasiliana na familia zao. al-Ansari amesema mateka watakaotoka familia moja watawekwa Pamoja katika kundi moja.

Kabla ya kuanza kutekelezwa mpango wa kuwekwa chini silaha, mapigano yaliendelea hata kwa kiwango kikubwa zaidi, huku ndege za kivita za Israel zikiyapiga maeneo Zaidi ya 300 nao wanajeshi wakikabiliana vikali karibu na kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Jiji la Gaza.

Hamas imesema watu 30 wameuawa katika shambulizi la Israel kwenye shule inayohusishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Wakimbizi – UNRWA eneo la Jabalia. Hakujawa na kauli yoyote kutoka kwa UNRWA.

dpa, reuters, ap, afp