1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushuru wa Donald Trump dhidi ya Umoja wa Ulaya Magazetini

Oumilkheir Hamidou
2 Mei 2018

Kitisho cha mzozo wa kibiashara kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya, tuhuma za waziri mkuu wa Israel dhidi ya mradi wa nyuklia wa Iran na siku ya wafanyakazi nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/2x0td
US-Präsident Donald Trump
Picha: picture-alliance/RS/MPI/Capital Pictures/M. Theiler

Tunaanzia Marekani ambako rais Donald Trump amerefusha kwa mwezi mmoja, hadi juni mosi muda wa kutangaza kama bidhaa za chuma puwa na bati zinazoagiziwa kutoka nchi za Umoja  wa Ulaya zitozwe ushuru au la. Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linazungumzia mvutano wa "ushuru wa kinga". Gazeti linaandika: "Vitisho, kiburi na kuwagonganishwa vichwa washirika-huo ndio mtindo wa kisiasa anaoupenda  rais wa Marekani Donald Trump. Tangu mwezi marchi nchi za Umoja wa ulaya na hasa Ujerumani inayotegemea mno biashara ya nje, zinajionea maudhi katika sera ya biashara, wakilazimika kumtegemea rais asiyekadirika wa Marekani Donald Trump . Matumaini ya kupatikana ufumbuzi wa kuziridhisha pande zote katika mzozo huu wa kibiashara, yamefifia baada ya kushindwa juhudi za kidiplomasia za kamishna wa Umoja wa Ulaya anaeshughulikia masuala ya biashara bibi Cecilia Malmström. Muhimu kwa Trump ni kimoja tu. Anataka kuitumia ridhaa ya nchi za Ulaya ili kuwaonyesha wapigakura wake nyumbani " anaweza kubadilisha kila kitu ulimwenguni."

Mtindo wa Trump unalingana na ule wa himaya ya warumi

Gazeti la Badische Zeitung linalinganisha mtindo wa Trump na ule uliokuwa ukitumika katika himaya ya  warumi mjini Roma. Gazeti linaendeelea kuandika: "Rais wa Marekani amewahurumia angalao kwasasa wazungu wa Umoja wa Ulaya. Hatowatoza bado ushuru kuwaadhibu. Hayo hayo yalikuwa yakifanyawa pia na warumi. Na wao pia walikuwa wakitanguliza mbele vitisho , lengo likiwa kulazimisha wapatiwe ridhaa. Silaha ya Trump ni soko ambalo hadi wakati huu lilikuwa wazi na muhimu zaidi hasa kwa makampuni ya Ujerumani-anataka kulifunga kwa kutumia ushuru. Hata katika kadhia nyengine Trump anatumia mtindo ule ule wa kale wa kudhibiti madaraka: Wagawe uwatawale ndio kauli mbiu yake."

Kitisho cha mzozo wa nuklea pamoja na Iran

Dhana za waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwamba Iran imeficha hati muhimu zinazoweza kutumiwa kutengeneza bomu la nyuklia zimechambuliwa kwa undani pia na wahariri wa magazeti ya Ujerumani. Gazeti la "Darmstädter linaonya dhidi ya kitisho cha mzozo wa kinuklia moja na Iran. Gazeti linaendelea kuandika: "Hujuma za kijeshi dhidi ya vituo vya Iran  zitaleta madhara yasiyokadirika na kuiudhi Urusi kupita kiasi. Dhana ambazo si mpya zisiwe chanzo cha balaa kama hilo. Kama dhana za Netanyahu zinabainisha mradi wa nyuklia wa Iran haukuwa wa amani kama Teheran inavyohoji, hiyo ni sababu mojawapo kubwa ya kutovunjwa makubaliano hayo na badala yake yarefushwe pamoja na kuishinikiza Iran iachane kabisa na fikra ya kuufufua mpango wake wa nyuklia, muda wa makubaliano haya ya sasa utakapomalizika  miaka saba kutoka sasa."

Hali ya wafanyakazi Ujerumani

Mada yetu ya mwisho magazetini inatupia jicho siku ya wafanyakazi. Gazeti la Volksstimme linaandika: "Shirikisho la vyama vya wafanakazi nchini Ujerumani DGB limeitumia mei mosi kuonya dhidi ya mtindo wa makampuni mengi kukwepa makubaliano ya pamoja kwa lengo la kuwalipa mishahara ya chini waajiriwa. Shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini Ujerumani linasema viwango vya mishahara ni vya chini mno ikilinganishwa na miaka ya 90 na kwamba thuluthi moja tu ya makampuni ndiyo yanayofuata muongozo wa makubaliano ya mishahara yanayofikiwa pamoja na vyama vya wafanyakazi."

 

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman