1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama wa Ulaya kuugubika mkutano wa usalama wa nyuklia

1 Aprili 2016

Uimarishwaji wa usalama wa bara la Ulaya linalokabiliwa na mashambulizi ya kigaidi, itakuwa ni moja ya ajenda itakayozingatiwa kwenye mkutano wa kilele kuhusu usalama wa nyuklia unaofanyika mjini Washington, Marekani.

https://p.dw.com/p/1INon
Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/J.Martin

Ikulu ya Marekani ina wasiwasi kwamba mashambulizi ya Paris, Ufaransa na Brussels, Ubelgiji yameonyesha udhaifu wa mashirika ya kijasusi ya Ulaya katika kupambana na mashambulizi ya wapiganaji wa jihadi kutoka Mashariki ya Kati.

Mshauri wa sera za kigeni wa Rais wa Marekani, Barack Obama, Ben Rhodes, amesema Marekani imepiga hatua katika mashambulizi ya anga na shinikizo dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu - IS, nchini Syria na Iraq.

Hapo jana Rais Obama mwenyeji wa mkutano huo, alizungumzia umuhimu wa ushirikiano kati ya Ulaya na Marekani, wenye lengo la kuwasambaratisha wapiganaji wa kigeni, kubaini uwezo wa mashambulizi hayo na kuacha kuwafadhili.

''Kutokana na mashambulizi ya Brussels, na kumbukumbu ya mauaji ya Paris, sio tu kuna uharaka mkubwa wa kuzungumzia suala la nyuklia, lakini kukomesha kabisa janga la ugaidi. Tunaendelea kuongeza ushirikiano wetu na Ufaransa katika juhudi za kupambana na ugaidi,'' alisema Rais Obama.

Obama akutana na viongozi wa Asia Mashariki

Mkutano huo wa kilele ulifunguliwa jana ambapo Rais Obama alizungumzia umuhimu wa ushirikiano kwenye sekta ya usalama miongoni mwa viongozi wa mataifa ya Asia Mashariki kuhusu namna ya kukabiliana na majaribio ya makombora na nyuklia yaliyofanywa hivi karibuni na Korea Kaskazini, ambayo amesema yanaongeza wasiwasi katika ukanda huo.

Rais Barack Obama na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan
Rais Barack Obama na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/dpa/K.Ozer

Pembezoni mwa mkutano huo, Rais Obama alikutana na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, Rais wa China, Xi Jinping pamoja na Rais wa Korea Kusini, Park Geun-Hye. Rais Obama alisema wanapaswa kuwa na msimamo wa pamoja katika juhudi zao kuzuia uchokozi unaofanywa na Korea Kaskazini na kuhakikisha eneo la Rasi ya Korea linakuwa salama na huru lisilo na silaha za nyuklia.

Wakati huo huo, Korea Kaskazini leo imefyatua kombora la masafa mafupi kuelekea baharini, saa chache baada ya Marekani, Korea Kusini na Japan kuahidi kushirikiana kwa karibu kuizua nchi hiyo kuendelea na mipango yake ya matumizi ya nyuklia na makombora.

Rais Obama pia amemuhakikishia Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kuhusu usalama wake, baada ya nchi hiyo kukumbwa na mfululizo wa mashambulizi ya mabomu.

Mkutano wa kilele kuhusu usalama wa nyuklia, unahudhuriwa na zaidi ya viongozi 50 wa mataifa na serikali pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa. Hata hivyo, mkutano huo haujahudhuriwa na Urusi, ambapo ni moja ya nchi inayomiliki asilimia nyingi ya silaha za nyuklia.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP,RTR,AP
Mhariri: Mohammed Khelef