1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meli 12 zaondoka Ukraine zikiwa na nafaka

31 Oktoba 2022

Meli 12 zilizobeba nafaka zimeng'oa nanga kwenye bandari za Ukraine, licha ya uamuzi wa Urusi kujitoa kwenye makubaliano ya kudhamini usafirisaji wa mazao kutoka ukanda wa vita.

https://p.dw.com/p/4Itde
Hafen von Odessa in der Ukraine
Picha: Metin Aktas/AA/picture alliance

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, meli hizo zimehusisha iliyopewa jina la African Robin iliyobeba ngano, SK Friendship iliyopakiwa maharage ya soya na Sealock iliyokuwa na njegere.

Umoja wa Mataifa umesema meli hizo ziliondoka Ukraine siku ya Jumapili kuelekea njia ya Bahari Nyeusi zikiwa pamoja na meli nyingine tatu.

Soma pia: Urusi yaendeleza mashambulizi miji ya Ukraine

Wizara ya Miundombinu ya Ukraine imesema meli yenye jina la Ikaria Angel, inayosafiri kwa namba ya shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, pia iliondoka ikiwa na mzigo wa nafaka wenye uzito wa tani 40,000 kuelekea nchini Ethiopia.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogn alisema Jumatatu kwamba nchi yake itaendeleza juhudi za kusafirisha nafaka kutoka Ukraine.

Ukraine Krieg | Seehafen Odessa
Meli ya kigeni ikiwasili katika bandari ya Odesa kupitia "njia ya nafaka" kusini mwa Ukraine.Picha: Yulii Zozulia/Ukrinform/abaca/picture alliance

Meli nyingine 16 zilikuwa zinapangiwa kuondoka kupitia njia salaama iliyokubaliwa leo, kwa mujibu wa mpango wa ujumbe kutoka Umoja wa Mataifa, Ukraine na Uturuki, uliosema Urusi ilikuwa imearifiwa kuhusu ratiba hiyo.

Urusi yasema kuendelea kusafirisha nafaka ni hatari

Urusi imesema itakuwa hatari kwa Ukraine kuendelea kusafirisha nafaka kupitia Bahari Nyeusi hivi sasa baada ya Moscow kusitisha ushiriki wake katika makubaliano hayo, huku msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, akilaumu vitendo vya upande wa Ukraine kwa kuvuruga makubaliano hayo.

"Katika mazingira ambapo Urusi inazungumza kuhusu kutowezekana kudhamini usalama wa usafiri wa meli katika maeneo hayo, makubaliano kama hayo hayawezekani, na yanachukuwa suura nyingine, ambayo ni hatari zaidi na yakikosa uhakikisho," alisema Peskov akizungumza na waandishi habari.

Soma pia: Putin asema hajutii kuivamia Ukraine

Mnamo mwezi Julai Urusi na Ukraine zilisaini muafaka ulioratibiwa na Uturuki na Umoja wa Mataifa, kuruhusu kurejea kwa usafirishaji wa nafaka uliositishwa na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Laiki Urusi ilisema siku ya Jumamosi kwamba ilikuwa inasitisha ushiriki wake katika makubaliano hayo baada ya shambulizi dhidi ya meli zake katika bahari Nyeusi. Ukraine imeishtumu Moscow kwa kuitishia njaa dunia.

BdTD | Türkei
Urusi na Ukraine ndiyo mataifa mawili yanayoongoza kwa uzalishaji wa nafaka duniani.Picha: Yasin Akgul/AFP

Peskov amesema Urusi ilikuwa inaendelea kuwa na mawasiliano ya kidiplomasia na Uturuki na Umoja wa Mataifa, lakini amekataa kusema chochote, alipoulizwa nini kinapaswa kutokea, kwa mtazamo wa Urusi, ili makubaliano hayo yaweze kurejelewa.

Hatua ya Urusi imesabisha ukosoaji kuanzia Ukraine, NATO, Umoja wa Ulaya na Marekani ambapo Rais Joe Biden aliitaja kuwa ya kikatili na kusema itaongeza vifo vitokanavyo na njaa.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blicken, aliituhumu Urusi kugeuza chakula kuwa silaha.

Chanzo: Mashirika