1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usafiri waparaganyika Ulaya kutokana na kimbunga Ciara

Sekione Kitojo
10 Februari 2020

Mamia ya safari za ndege na huduma za treni zimefutwa  kaskazini magharibi mwa Ulaya leo wakati upepo mkali wa kimbunga Ciara,hapa Ujerumani kikitambulika kama kimbunga Sabine kikishambulia maeneo ya Ulaya. 

https://p.dw.com/p/3XWh9
Deutschland Sturmtief Sabine | Köln
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kusch

Maeneo  ya  kaskazini  mwa  Ufaransa  yamewekwa  katika tahadhari  ya  juu ambapo  watu  wameshauriwa  kuepuka  kwenda pwani  kutokana  na  uwezekano  wa  athari  za   upepo  mkali wa kimbunga hicho. Uingereza, ambayo  imekumbwa  na  upepo  huo mkali jana  Jumapili  pamoja  na  mafuriko makubwa  katika  eneo  la kaskazini  mwa  nchi  hiyo, inaendelea  kuwa  katika  hali ya tahadhari  wakati ofisi  ya  utabiri  wa  hali  ya  hewa  ikionya kuhusu  upepo  mkali, mvua  kubwa  na  theluji.

Deutschland Sturmtief Sabine | Essen
Miti imeangushwa chini na upepo mkali Ciara ama kwa jina jingine SabinePicha: picture-alliance/dpa/Feuerwehr Essen/M. Filzen

"Wakati kimbunga  Ciara  kinatoweka, hii  haina  maana  kwamba tunaingia  katika  kipindi cha  utulivu wa  hali  ya  hewa," afisa wa idara ya  utabiri wa  hali  ya  hewa  Alex Burkill  amesema.

Kasi ya juu  ya  upepo iliyorekodiwa  ilikuwa  kilometa 150 kwa saa katika  kijiji  cha kaskazini  magharibi  mwa  Wales  cha  Aberdaron.

Safari  kadhaa  za ndege  zimefutwa  ama  kucheleweshwa  na makampuni  ya  safari  za  treni  yamewataka  wasafiri  kutosafiri  na wameruhusu  safari  chache pamoja  na  kudhibiti  kasi ya  mwendo.

Deutschland: Auswirkungen des Sturmtiefs "Sabine" - Dortmund
Wasafiri wakiwa wamekwama katika kituo kikuu cha treni mjini DortmundPicha: Getty Images/AFP/I. Fassbender

Huduma ya  feri  kati ya  Dover kusini mashariki mwa Uingereza na mji  wa  bandari  nchini  Ufaransa  wa  Calais zimesitishwa  jana hadi itakapotolewa  taarifa  nyingine.

Nyumba  kadhaa  zakosa umeme

Nchini  Ireland, ambako  tahadhari  ilikuwa  katika kiwango cha  rangi ya  chungwa, ambayo  haijafikia  kiwango cha  juu  kabisa, kutokana na  hatari ya  mafuriko katika  maeneo  ya  pwani, nyumba  10,000, mashamba  na  biashara  zimekuwa  hazina  umeme.

Ubelgiji  pia  ilikuwa  katika  tahadhari  na  kiasi  ya  safari 60 za ndege  kwenda  na  kutoka  Brussels  zilifutwa. Katika  mji  huo, miti na vyuma  vinavyotumiwa kusaidia  katika  ujenzi  wa  majengo viliondolewa  na  upepo na  baadhi  ya  majengo kuharibiwa lakini hakuna  mtu  aliyefariki.

Nchini  Ujerumani, huduma  za  treni za  kwenda  mbali  zilisitishwa. Upepo wa  kimbunga  ulikuwa  mkali  sana , na  tukalazimika kusitisha  kabisa  safari  za  treni za  mbali  nchini  Ujerumani  siku ya  Jumapili," Msemaji  wa  shirika  la  reli  nchini  Ujerumani Deutsche Bahn, Achim Stauss aliliambia  shirika  la  habari  la  AFP.

Mönchengladbach: Sturmtief "Sabine" - Derby abgesagt
Shabiki wa kandanda wa klabu ya Moenchengladbach akiangalia pambano la klabu yake na FC Koln limefutwaPicha: picture-alliance/dpa/R. Weihrauch

Viwanja  kadhaa  vya  ndege  nchini  Ujerumani  vimelazimika  kufuta safari  wakati kimbunga  hicho  kikipita  katika  eneo  la  kaskazini. Viwanja vya  ndege  vya  Frankfurt, Munich, Kolon  na  Hannover  vilikuwa  miongoni  mwa  vilivyoathirika, wakati  katika uwanja  wa  Duesseldorf, safari 120 zilifutwa.

Mchezo wa kandanda wa  Bundesliga kati ya mahasimu wa jadi Borussia  Moenchengladbach dhidi ya  FC Kolon umefutwa jana kutokana  na  hatari ya  kimbunga  hicho.