1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yatishia kuendelea kuwauwa 'magaidi' Syria

Daniel Gakuba
6 Septemba 2018

Urusi imesema itaendelea kuwauwa 'magaidi' jimboni Idlib na kwingineko Syria, hadi nchi hiyo itakapopata amani. Hayo yanajiri wakati hofu ukiongezeka kuhusu uwezekano wa mashambulizi makubwa katika jimbo la Idlib.

https://p.dw.com/p/34RRp
Syrien Russische Luftangriffe nahe Idlib
Baadhi ya maeneo ya Idlib yamekuwa yakikabiliwa na mashambulizi ya mizinga na ya angaPicha: Getty Images/AFP/O. H. Kadour

 

Kauli hiyo nzito imetolewa mapema leo na msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Urusi Maria Zakharova, na kuripotiwa na mashirika ya habari ya Urusi. Msemaji huyo amesema kuwauwa wale aliowaita magaidi nchini Syria, si suala la usalama wa taifa la Urusi.

Idlib ni jimbo la mwisho linaloshikiliwa na waasi nchini Syria, ambalo linakaliwa na mchanganyiko wa makundi ya upinzani, yakiwemo yale yaliyoorodheshwa na mataifa makubwa kama makundi ya kigaidi.

Mashambulizi ya kutumia mabomu hapa na pale yamekuwa yakiyalenga makundi yenye silaha mnamo siku za hivi karibuni, na mapema leo sehemu ya Kusini Mashariki mwa jimbo hilo imepigwa kwa mizinga ya majeshi ya serikali ya Syria, na kushambuliwa kutoka angani na ndege za Urusi.

Marais wa Urusi, Iran na Uturuki wajiandaa kukutana

Syrien Rebellen in Idlib-Provinz
Wapiganaji wa waasi wamejiweka katika hali ya tahadhari wakisubiri mashambulizi ya serikali.Picha: Getty Images/AFP/O.H. Kadour

Wakati hayo yakijiri, marais wa Urusi, Iran na Uturuki wanajiandaa kukutana mjini Tehran, kujaribu kuepusha mapigano makubwa jimboni Idlib. Mevlut Cavusoglu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ambayo inaunga mkono baadhi ya makundi ya waasi yalioko Idlib, amesema wamekuwa wakijaribu kuepusha janga la umwagaji damu, tangu uwezekani wa mashambulizi dhidi ya Idlib ulipodhihirika.

'Ni wazi kwamba utawala wa Syria unataka kufanya mashambulizi dhidi ya Idlib, na utawala huo unao wafadhili; Urusi na Iran. Kwa hiyo, tutaendelea kuzungumza na Urusi na Iran', amesema Cavusoglu.

Duru kadhaa za mazungumzo zimeambulia patupu katika juhudi za kusuluhisha vita nchini Syria, ambavyo vimedumu kwa zaidi ya miaka saba, na kuangamiza maisha ya watu zaidi ya 350,000.

Wanaofuatilia kwa karibu mzozo huo wanasema janga jingine linaweza kuepukwa, ikiwa Uturuki itaihakikishia Urusi hali ya utulivu, na Urusi yenyewe ikitambua kwamba mzozo mkubwa zaidi jimboni Idlib unakwenda kinyume na maslahi yake kisiasa.

Raia waanza kuyapa kisogo makazi yao

Infografik Karte Streitkräfte im Idlib-Region Syrien EN
Mkoa wa Idlib unakaliwa na makundi mengi ya waasi

Raia waliojawa na hofu wameanza kulikimbia jimbo hilo kabla ya kuanza kwa mashambulizi kamili. Shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza waliokimbia wanakadiriwa kuwa mamia kadhaa. Ripoti ya shirika hilo imesema ndege za Urusi zimeuwa raia wasiopungua 9, wakiwemo watoto watano kutoka familia moja, na kwamba raia wengine 10 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo. Jeshi la Urusi limethibibitisha kwamba ndege zake zimelishambulia kundi la al-Nusra Front.

Hata hivyo idadi ya watu walioyakimbia makazi yao bado ni ndogo ikilinganishwa na makadirio ya Umoja wa Mataifa, ambao unahofu kwamba watu zaidi ya 800,000 wanaweza kushika njia ya kwenda ukimbizi.

Mkuu wa shirika la kuchunguza haki za binadamu Syria Abdel Rahman, amesema familia zipatazo 180 zenye watu takriban 1000 zimeziacha nyumba zao, na mwandishi wa AFP amesema ameshuhudia msafara wa familia nyingi ukielekea Kaskazini karibu na mpaka wa Uturuki.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe,rtre

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman