1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yatangaza kuyanyakua rasmi majimbo ya manne ya Ukraine

30 Septemba 2022

Rais Vladimir Putin wa Urusi hii leo amesaini mikataba ya kuyachukua majimbo yanayoyakaliwa kimabavu na jeshi lake nchini Ukraine na kusema atatumia kila njia kuyalinda maeneo hayo ambayo Ukraine na mataifa ya Magharibi wanasema yamechukuliwa kwa njia isiyo halali inayokiuka sheria za kimataifa.

https://p.dw.com/p/4HbVq

Kwenye hotuba kabla ya kutia saini makubaliano hayo, Putin aliiomba Ukraine kukubali mazungumzo ya kumaliza vita nchini humo vilivyodumu kwa miezi saba sasa.

Sherehe za kuyachukua majimbo hayo zinafanyika siku tatu baada ya kumalizika kwa kile kinachoitwa kura ya maoni iliyoandaliwa na Urusi ya kuyachukua maeneo hayo huku Putin akitolea mwito Ukraine kuheshimu matokeo hayo na kuonya kamwe Urusi haitayarejesha majimbo hayo. 

Katika ripoti hii unaweza pia kusikiliza mahojiano kati ya John Juma na  mchambuzi wa siasa za kimataifa Abdalla Mzee akiwa Berlin juu ya hatua ya Urusi kuyanyakua majimbo ya Ukraine.

Ukraine-Krieg | Wolodymyr Selenskyj
Rais Volodmyr Zelensky wa Ukraine Picha: Ukraine Presidential Press Service/AFP

Wakati hayo yakijiri rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema taifa lake linawasilisha pendekezo la kuharakishwa kwa ombi lake la kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Ameyatoa matamshi hayo mara baada ya Urusi kusema itayachukua majimbo yake manne iliyoadhibiti wakati vita vikiendelea nchini Ukraine na Urusi kuitisha kile ilichoita kura ya maoni ambayo jamii ya kimataifa inaona kuwa siyo halali.

Zelensky amesema wanachukua hatua ya kusaini ombi la Ukraine la kuharakishwa kwa pendekezo lao la kujiunga na NATO.

Aidha Zelensky ameonya kwamba hataingia kwenye mazungumzo na Urusi iwapo rais Vladimir Putin atakuwa madarakani na kusema kwamba atakubali kuzungumza na rais mpya.

Kyiv na mataifa ya Magharibi wamepinga unyakuaji wa maeneo nchini Ukrainewakati Umoja wa Ulaya ukitangaza kutoitambua kura hiyo iliyoielezea kama hatua ya Urusi ya kuingilia zaidi uhuru wa Ukraine.

Mapigano bado yanaendelea kati ya Urusi na Ukraine

Mapema leo Ukraine na Urusi zimeshutumiana kuhusika na mashambulizi ya makombora kwenye msafara wa magari ya kiraia katika eneo la kusini mwa Zaporizhzhia na kusababisha vifo vya watu takriban 23 na kuwajeruhi wengine 28. 

Russische Militäraktion in der Ukraine
Picha: Sofiia Gatilova/REUTERS

Msafara huo uliokuwa umebeba raia na vifaa ulishambuliwa karibu na mji wa kusini mwa Ukraine unaokaliwa na vikosi vya Urusi wa Zaporizhzhia. 

Gavana wa Mkoa wa Zaporizhzhia Oleksandr Starukh amesema shambulio hilo limeendeshwa na majeshi ya Urusi na hivo kusababisho vifo vya watu 28, ambao wote ni wakazi wa eneo hilo.

Naye Vladimir Rogov, Afisa anayeiunga mkono Kremlin akiilaumu Kiev kwa uchochezi na kukanusha kuwa jeshi la Urusi lilihusika na shambulio hilo.

Eneo la kiwanda cha Zaporizhzhia, lililokuwa na wakazi 700,000 kabla ya vita, liko chini ya udhibiti wa Ukraine lakini limekuwa likikabiliwa na mashambulizi ya Urusi.

Aidha, shirika la habari la serikali ya Urusi limebaini kuwa Afisa aliyeteuliwa na Moscow huko Kherson, eneo la kusini mwa Ukraine linalodhibitiwa na Urusi, ameuawa katika mashambulizi ya vikosi vya Kiev.