1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yasababisha wasiwasi wa silaha za Nyuklia

15 Machi 2022

Hatua ya rais Putin ya kukiweka tayari kikosi chake cha silaha za Nyuklia yairudisha kwenye ramani alama ya vita baridi

https://p.dw.com/p/48Ukj
BG Nuklearwaffen | Pakistan Hatf-VI (Shaheen-2) Rakete
Picha: ISPR HO/epa/dpa/picture-alliance

Silaha za Nyuklia zilikuwa alama ya vita baridi. Kitisho cha hivi sasa kinachotokana na Urusi iliyoko vitani nchini Ukraine kimeirudisha tena kumbukumbu hiyo kwenye ramani  kwa watu wengi. Je ni kwa namna gani hili linaweza kuzuiwa na Ulaya ina kinga aina gani?

Trident Ii I D-5 Missile I U-Boot-gestützte ballistische Rakete
Picha: Getty Images

Wakati rais wa Urusi Vladmir Putin alivyotowa amri ya kukitaka  kikosi chake maalum chenye  uwezo wa kutumia silaha za Nyuklia kukaa tayari,mwanzoni mwa vita vya Ukraine,Ulaya ilipata mshtuko.

Mwanzoni mwa mwezi huu wa March Putin alichukua hatua nyingine ya kupeleka  nyambizi zilizotengenezwa Urusi za  kubeba silaha za Nyuklia pamoja na makombora yenye uwezo wa kuhamishwa katika luteka za kijeshi. Suali hapa ni je kiongozi huyo wa Urusi alikuwa akitoa kitisho cha kufanya shambulio la kutumia silaha za Nyuklia?

Ikiwa na zaidi ya vichwa 6,300 vya Nyuklia,Urusi ndio nchi yenye kumiliki idadi kubwa ya silaha za Nyuklia duniani. Ndani ya Jumuiya ya kujihami ya NATO,Marekani ndiyo nchi yenye idadi kubwa ya silaha za Nyuklia ikiwa na vichwa 5,800 vya silaha hizo za maangamizi.

Ufaransa inatajwa kumiliki kiasi vichwa 300 vya Nyuklia wakati Uingereza ikidaiwa kuwa na kiasi 215,ingawa idadi jumla ya silaha hizo haijulikani kutokana na mataifa mengi  yanayotajwa yanaweka taarifa zao nyingi kuwa siri kuhusiana na miradi yao ya Nyuklia.

Bila ya dhima ya Marekani katika muungano wa kuzitetea nchi zisokuwa na uwezo wa silaha hizo za Nyuklia,nchi za Ulaya haziwezi kuzuia shambulizi la Nyuklia kwa kutumia nguvu za kijeshi. Muungano huo umejengeka kwa msingi uliotilia maanani kwamba hakuna nchi inayoweza kuthubutu kuishambulia nchi yoyote ya Jumuiya ya kujihami ya NATO kwa silaha za Nyuklia kwasababu nchi hiyo italazimika kutarajia shambulizi  la  kuikabili.

Brüssel NATO Gipfeltreffen l Generalsekretär Stoltenberg
Picha: Kenzo Tribouillard/AFP

Lakini pia ifahamike kwamba nchi zenye nguvu za Nyuklia katika muungano wa kijeshi wa NATO zinatafautiana kabisa katika kuchukua hatua ya  kuzuia mashambulizi. Ufaransa na Uingereza zinategemea kile kinachoitwa hatua ya wastani ya kuzuia shambulizi la Nyuklia.Nchi hizi zinaamini katika kulipiza au kumzuia adui kwa kumpya onyo la mwisho na hasa Ufaransa.

Kwa upande mwingine Marekani iko tafauti inaamini katika kutumia silaha za Nyuklia lakini kwa kupunguza nguvu za mripuko kuepusha madhara makubwa.Kimtazamo wa kisheria ni kosa kutumia silaha yoyote ya Nyuklia yenye uwezo wa kusababisha madhara makubwa dhidi ya raia,ni kosa linalokiuka sheria ya kimataifa ya kusimamia misingi ya kiutu.

Großbritannien | Sicherheitsprobleme | Britische Atomfabrik
Picha: Tony Harris/dpa/picture alliance

Rais wa Marekani ndie mtu wa kwanza anayepaswa kuamua kuhusu matumizi ya silaha za Nyuklia za nchi hiyo zilizowekwa nchini Ujerumani,Itali,Ubelgiji na Uholanzi. Anatakiwa kutowa idhini ya kuachiwa mabomu hayo na nchi yanakopelekwa itabidi iridhie mabomu hayo yarushwe na ndege zake za kivita.

Na kabla ya hatua hiyo kuchukuliwa,wanachama wengine wa NATO watabidi kushauriana na chombo kikuu cha maamuzi ya msingi ya kisiasa cha jumuiya hiyo  NAC.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW