1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaonya dhidi ya uwezekano wa vita vya tatu vya dunia

Saleh Mwanamilongo
13 Oktoba 2022

Huku mawaziri wa ulinzi wa nchi za jumuiya ya kujihami, NATO, wakikutana mjini Brussels, Urusi imeonya kwamba kuijumuisha Ukraine katika Muungano wa kujihami wa NATO kunaweza kuanzisha Vita vya Tatu vya Dunia.

https://p.dw.com/p/4I7h5
China Flugzeugträger Liaoning der Volksbefreiungsarmee
Picha: AFP

Naibu katibu wa Baraza la Usalama la Urusi, Alexander Venediktov, amesema leo kwamba kukubalika kwa Ukraine katika muungano wa NATO kunaweza kusababisha vita vya tatu vya dunia.

Kwenye mahojiano na shirika la habari la serikali TASS, Venediktov amesema serikali ya Kyiv inafahamu vyema kuwa hatua kama hiyo itamaanisha kuongezeka kwa uhakika wa Vita vya Tatu vya Dunia, alinukuliwa pia akisema asili ya kujiua ya hatua kama hiyo inaeleweka na Wanachama wenyewe wa NATO.Venediktov, ambaye ni mshirika mkubwa wa Rais Putin, alisema anahisi maombi ya Ukraine kujiunga na NATO yalikuwa propaganda.

''Tutatoa mifumo zaidi ya ulinzi wa anga''

Katibu MKuu wa jumuiya ya NATO, Jens Stoltenberg amesema Nato itaendelea kusimama na Ukraine.

''Tutaongeza msaada wetu na hasa, tutatoa mifumo zaidi ya ulinzi wa anga kwa Ukraine. Pia nakaribisha ujumbe mzito kutoka kwa jumuiya ya kimataifa uliotolewa hapo jana. Kura hiyo katika Umoja wa Mataifa ililaani wazi unyakuzi haramu wa maeneo ya Ukraine na wito wa wazi kwa Urusi, Rais Putin kubadili maamuzi haya na kuheshimu mamlaka ya mipaka ya Ukraine." alisema Stoltenberg.

Kuna umakini wa vitisho vya Urusi ?

Kombora la masafa mafupi la Tochka likirushwa April,2000 mjini Kaliningrad, Urusi
Kombora la masafa mafupi la Tochka likirushwa April,2000 mjini Kaliningrad, UrusiPicha: Igor Sarembo/dpa/picture alliance

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Christine Lambrecht alionya dhidi ya kuchukulia kwa urahisi vitisho vya nyuklia vya Urusi katika vita vya Ukraine. Kando ya mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa NATO mjini Brussels, Lambrecht amesema ni muhimu sana kuchukua vitisho hivyo kwa umakini na kuwataka wanachama wa jumuiya hiyo kuwajibika ipasavyo.

Huku hayo yakijiri, Rais wa Uturuki Recep Erdogan amesema nchi yake inalenga kukomesha haraka iwezekanavyo umwagaji damu katika vita kati ya Urusi na Ukraine licha ya kuwepo vikwazo lukuki. Rais huyo wa Uturuki amesisitiza pia kuwa amani inaweza kupatikana kupitia diplomasia.

Mashambulizi mapya ya Urusi

Nchini Ukraine kwenyewe, mamlaka zimesema leo kuwa makombora ya Urusi yameipiga zaidi ya miji 40,ukiwemo mji wa bandari wa Mykholaiv. Awali rais Ukraine Volodymir Zelensky alisema wanajeshi wake wametwaa tena eneo la kusini na kukaribisha ahadi ya Magharibi ya kuwasilisha mifumo ya ulinzi wa anga huko Kyiv.

Taarifa hii imetolewa baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupiga kura na kutangaza kuwa unyakuzi wa Moscow wa maeneo ya Kusini na Mashariki mwa Ukraine ni batili.