1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Urusi yamkamata mkosoaji mwingine wa Kremlin

2 Juni 2021

Polisi ya Urusi imemkamata Dmitry Gudkov mmoja ya wakosoaji wakubwa wa ikulu ya Kremlin na taarifa zinasema huenda atakabiliwa na kifungo jela.

https://p.dw.com/p/3uJhM
Russland Moskau | Aktivist Dmitri Gudkow
Dmitri Gudkov mkosoaji mkubwa wa rais Vladmir Putin wa Urusi Picha: Alexander Shcherbak/TASS/imago images

 Taarifa za kukamatwa kwa Gudkov zimethibitishwa na baba yake mzazi aliyesema kuwa alikamatwa baada ya msako wa polisi  kwa madai ya kutolipa kodi ya nyumba tangu mwaka 2015.

Baba wa Gudkov, aitwaye Gennady aliandika kupitia ukurasa wa Twitter taarifa za kukamatwa kwa mwanaye akisema kundi la watu waovu limekamata hatamu za uongozi nchini Urusi na linawatesa watu wa kawaida.

Mapema jana polisi ilifanya upekezi kwenye makaazi ya Gudkov yaliyopo nje kidogo ya mji wa Moscow pamoja na kwenye nyumba za ndugu na jamaa wa mkosoaji huyo.

Ikiwa atapatikana na hatia ya madai hayo ya kukwepa kodi, Gudkov anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 5 gerezani.

Gudkov mwanasiasa mwiba kwa rais Putin

Russland Präsident Wladimir Putin
Rais Vladimir Putin wa Urusi Picha: Sertgei Ilyin/Pool Sputnik Kremlin/AP/dpa/picture alliance

Gudkov ni mwanasiasa na mbunge wa zamani wa upinzani ambaye kwa muda mrefu amekuwa mwiba mchungu kwa utawala wa rais Vladimir Putin.

Mwaka 2003 wakati akiwa mbunge katika Braza la Wawakilishi la Urusi, Gudkov alifukuzwa kutoka chama cha Just Russia kinachoonga mkono sera za rais Vladimir Putin kwa kutoa msaada wa kuandaliwa maandamano ya umma dhidi ya serikali ya Urusi.

Baadae mwanasiasa huyo alijiunga na chama cha upinzani cha kiliberali nchini Urusi na kuendesha kampeni kubwa ya kumpinga rais Putin.

Kukamatwa kwa Gudkov mwenye umri wa miaka 41 kunakuja siku moja tangu polisi ya Urusi ilipomkamata mkosoaji mwingine wa serikali  Andrei Pivovarov, kwa kumshusha kutoka kwenye ndege iliyokaribia kuanza safari.

Kushikiliwa kwa Gudkov na  Pivovarov ni matukio ya karibuni kabisa ya kile wakosoaji wa ikulu ya Kremlin wanakitaja kuwakampeni ya vitisho dhidi ya wapinzani wa rais Vladimir Putin kuelekea uchaguzi wa Bunge wa mwezi Septemba.

Umoja wa Ulaya na Amnesty wataka kuachiwa kwa Povovarov 

Ama kuhusu kushikiliwa kwa Pivovarov, polisi imesema ni kwa sababu ya uchunguzi wa jinai unaomuhusisha mwanaharakati huyo na kile mamlaka mjini Moscow zimekitaja kuwa "taasisi isiyokubalika"

Russland Oppositionsführer Alexej Nawalny
Alexei Navalny Picha: Babuskinsky District Court/AP/dpa/picture alliance

Pivovarov ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa asasi ya kupigania demokrasia iliyopigwa marufuku ya Open Russia anakabiliwa na kifungo cha miaka 6 iwapo atakutwa na hatia.

Kukamatwa kwake kumechochea lawama kutoka Umoja wa Ulaya uliotaka aachiwe huru haraka na  ukisema kesi dhidi yake inadhihirisha ukandamizaji unaoendelea dhidi ya asasi za kiraia, wanasiasa wa upinzani na vyombo vya habari.

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International pia nalo limetoa wito wa kuachiwa huru kwa Pivovarov.

Hayo yote yanajiri wakati mkosoaji mwingine mkubwa na kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny alihukumiwa kifungo cha miaka mwili jela mwezi Februari kwa madai yaleyale kuwautawala wa Putin unawalenga wapinzani na wanaharakati wanaoupinga.