1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yakanusha kutoa silaha za kemikali kwa Syria

MjahidA21 Agosti 2012

Siku moja baada ya Rais wa Marekani Barrack Obama kuionya Syria kuwa itakuwa imevuka mipaka iwapo itaamua kutumia silaha za kemikali kwa upinzani, Urusi imekanusha vikali hatua ya kutoa silaha hizo kwa Syria.

https://p.dw.com/p/15tqW
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei LavrovPicha: picture-alliance/dpa

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema urusi kamwe haijauza silaha hizo kwa Syria. Lavrov amesema mataifa ya magharibi hayapaswi kuingilia mambo ya ndani ya Syria badala yake yanapaswa tu kushinikiza kuwepo kwa mazungumzo ya kuleta amani nchini humo.

Kwa upande wake mkurugenzi wa shirika la uangalizi wa silaha za nyuklia wa Urusi kanali Vladimir Mandych, amesema kwa sasa hawezi kutamka iwapo silaha za kemikali zinazomilikiwa na Syria ni kutoka Urusi lakini amesema taifa hilo halijawahi kutoa silaha hizo kwa Syria. Wakati huo huo, Mandych ametoa onyo duniani kote kwamba mikakati thabiti inapaswa kuchukuliwa ili silaha kama hizi zisiwahi kutumika katika karne hii ya 21.

Kanali Vladimir Mandych, amesema matumizi ya silaha hizo, huweza kusababisha uharibifu mkubwa wa kimazingira na pia athari kubwa kwa binaadamu.

Matamshi hayo yamekuja baada ya Rais wa Marekani Barack Obama kutoa onyo kuwa iwapo Syria itatumia kemikali hizo kwa upinzani, basi itamlazimu kufikiria tena swala la kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Syria.

Hata hivyo serikali ya Syria imesema haitatumia silaha hizo kwa waandamanaji lakini ikatishia kuzitumia iwapo mataifa ya nje yatajiingiza kijeshi nchini humo. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema eneo zima la Mashariki ya kati litakuwa hatarini iwapo Syria itaamua kufanya hivyo.

Westerwelle ameuomba utawala wa Rais Bashar Al Assad kutofanyia dhihaka suala hili. Huku hayo yakiarifiwa mapigano makali bado yanaendelea nchini Syria. Gari moja lililokuwa limeegeshwa karibu na vituo vya ukaguzi wa kijeshi, mashariki mwa mji wa al-Mazzeh liliripuka na kusababisha vifo vya wanajeshi 4 huku wengine 6 wakijeruhiwa.

Kituo cha ukaguzi wa kijeshi, Syria
Kituo cha ukaguzi wa kijeshi, SyriaPicha: dapd

Na katika mji mkuu wa Syria, Damascus, shirika la kutetea haki za binaadamu limesema maiti 12 ambazo mpaka sasa hazijatambuliwa zilipatikana katika kitongoji cha Qaboon. Watoto wawili ni miongoni mwa miili hiyo iliopatikana. Hapo jana wanaharakati waliripoti kuuwawa kwa watu 200 mjini Allepo akiwemo muandishi habari mmoja raia wa Japan aliye na umri wa miaka 45, Mika Yamamoto.

Mika alipigwa risasi shingoni alipokuwa akifuatilia habari ya utawala usiomuunga mkono rais Assad waliposhambuliwa na vikosi vya rais Assad mjini Allepo. Kifo chake kinaongeza idadi ya waandishi wa kigeni waliouwawa nchini humo kufikia wanne baada ya kuuwawa kwa waandishi wawili wa kifaransa na Mmarekani mmoja. Kifo chake kilithibitishwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Japan.

Waasi wanaopigana na jeshi la Bashar Al Assad ni kutoka kwa madhehebu ya Wassuni huku Assad akitokea madhehebu ya Alawi. Sasa vita hivyo vya kikabila vimesambaa nchini Lebanon baada ya watu wawili kuuwawa na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa mjini Tripoli nchini humo.

Mwandishi Amina Abubakar/dpa/ AFP/Reuters

Mhariri Josephat Charo