1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yaituhumu Marekani kupanga shambulizi ikulu ya Kremlin

4 Mei 2023

Urusi imeishutumu Marekani kwa kupanga shambulizi la droni dhidi ya ikulu ya rais Vladimir Putin, na kwamba hujuma ya Ukraine dhidi ya Urusi imepitiliza.

https://p.dw.com/p/4QuYj
Droni karibu na jengo la Ikulu ya Kremlin mjini Moscow
Picha ikionesha Droni ikikaribia jengo la Ikulu ya Kremlin mjini Moscow Picha: Ostorozhno Novosti/REUTERS

Urusi imedai shambulizi hilo lilikuwa jaribio la Ukraine kutaka kumuua rais Putin.

Msemaji wa serikali ya Urusi Dmitry Peskov amesema, maamuzi ya kufanya mashambulizi kama hayo hayafanywi na Ukraine bali Marekani, na kwamba Ukraine hufanya tu kile inachoambiwa kufanya.

Marekani tayari imekanusha vikali shutuma hizo, huku msemaji wa Ikulu ya White House John Kirby akisema Peskov anasema uwongo. Ukraine vilevile imekanusha kuhusika.

Siku moja tu baada ya kisa hicho na Urusi kusema itajibu vikali, Urusi imefanya mashambulizi ya droni usiku kucha dhidi ya Ukraine kwa kutumia ndege zisizokuwa na rubani.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ameitahadharisha Urusi kutotumia madai ya shambulizi hilo la droni kuzidisha mgogoro wake na Ukraine.