1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yaishambulia kwa droni na makombora Ukraine.

26 Agosti 2024

Urusi imeishambulia Ukraine kwa makombora na droni ikilenga miundo mbinu ya nishati katika mikoa 15 ikiwa ni pamoja na mji mkuu Kiev. Ukraine inawaomba washirika wake waisaidie kudhibiti mashambulizi ya Urusi.

https://p.dw.com/p/4jvD5
Mkoa wa  Odessa baada ya shambulio la Urusi
Wazima moto wakijaribu kuzima moto Odessa baada ya shambulio la UrusiPicha: Press Service of the State Emergency Service of Ukraine in Odesa region/Handout/REUTERS

Urusi imefanya mashambulizi makubwa ya droni na makombora dhidi ya Ukraine leo Jumatatu, yaliyolenga miundo mbinu ya nishati kote nchini humo. Takriban watu watatu wameripotiwa kuuwawa. Kwa upande mwingine serikali mjini Kiev imesema wanajeshi wa Belarus ambayo ni mshirika wa Urusi wako katika eneo la mpakani  na Ukraine.Soma Pia: Marekani yatahadharisha uwezekano wa mashambulizi ya Urusi

Taarifa zilitolewa na maafisa wa Ukraine leo asubuhi zilieleza kwamba miundo mbinu ya nishati katika alau miko mitatu ya nchi hiyo imeshambuliwa na Urusi,mikoa hiyo ni Zaporizhzhia,Rivne na Lviv.

Mifumo ya kurusha roketi ya Ukraine
Mifumo ya kuyetuwa roketi ya Ukraine aina ya Neptune R-360Picha: Depositphotos/IMAGO

Uharibifu wa mashambulizi ya Urusi,dhidi ya Ukraine

Imeelezwa kwamba Urusi imerusha  makombora kwa wingi na droni kote kwenye maeneo hayo na watu wasiopunguwa watatu wameuwawa huku umeme ukikatika kote nchini Ukraine.

Mashambulizi hayo yalianza usiku wa kuamkia leo na kuendelea hadi asubuhi katika kile ambacho kinaonesha kuwa mashambulio makubwa zaidi kuwahi kufanywa na Urusi dhidi ya Ukraine katika kipindi cha wiki kadhaa.

Waziri mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal leo asubuhi akielezea juu ya matukio yaliyoshuhudiwa amethibitisha kwamba wanajeshi wa Urusi wamerusha droni,na kushambulia pia kwa makombora ya masafa marefu aina ya Kinzhal katika majimbo 15 ambayo ni nusu ya nchi nzima.

Amesema uharibifu mkubwa umefanyika katika majimbo kadhaa na kwa bahati mbaya mashambulizi hayo yalilenga hasa miundo mbinu ya nishati.Shirika la umeme la Ukraine Ukrenergo limelazimika kukata nguvu za umeme nchini humo ili kurekebisha mfumo mzima wa kusambaza umeme.

Rais Zelensky aomba silaha kwa washirika

Kutokana na kupamba moto kwa mashambulio ya Urusi, Rais Volodymry Zelensky amewatolea  washirika wake kuipatia nchi yake makombora ya masafa marefu pamoja na idhini ya kuzitumia silaha hizo kushambulia ndani ya ardhi ya Urusi.

Jaribio la roketi aina ya Vilkha-M  la Ukraine
Jaribio la roketi aina ya Vilkha-M la Ukraine Picha: Ukrinform/dpa/picture-alliance

Nikinukuu kauli ya Zelensky amesema, Ili kuzima mashambulizi ya kikatili dhidi ya miji ya Ukraine kuna haja ya kuyasambaratisha maeneo yanakotokea makombora ya Urusi.Tunategemea msaada wa washirika wetu na bila shaka tutaitia adabu Urusi.

Kwa mujibu wa jeshi la anga la UKraine droni chungunzima za Urusi zilizorushwa kwa makundi zilielekezwa maeneo ya mashariki,Kaskazini na Kusini pamoja na mikoa ya kati ya Ukraine na kisha zikafuatiwa na mashambulio ya makombora ya masafa ya kati na marefu.

Miripuko mikubwa ilisikika katika mji mkuu Kiev huku umeme na usambazaji wa maji ukikatika katika mji huo,kwa mujibu wa meya Vitali Klitschko.Taarifa pia zimeleeza mifumo ya ulinzi wa anga ya Ukraine ilifanikiwa kuziharibu droni 15 na makombora 15 yaliyoulenga mji huo wa Kiev.

Ukraine Luzk, baada ya makaazi ya watu kushambuliwa kwa droni
Baada ya shambulio la droni kulenga makaazi ya watu mji wa LuzkPicha: Press Service of the State Emergency Service of Ukraine in Volyn region/Handout/REUTERS

Kadhalika makaazi ya watu yaliharibiwa vibaya katika mikoa mbali mbali ya Ukraine, kuanzia Sumy ulioko mashariki hadi mikoa ya Mykolaiv na  Odesa iliyoko Kusini mpaka  Rivne ambako ni Magharibi mwa nchi hiyo.

Belarus yapeleka wanajeshi mpakani mwa Ukraine

Wakati huo huo, Ukraine imethitisha kwamba wanajeshi wa Belarus wameshaanza kujikusanya  katika eneo la mpakani na nchi hiyo ikiwa ni wiki moja tu baada ya nchi hiyo mshirika wa Urusi kutangaza itachukuwa hatua hiyo.

Wizara ya mambo ya nje ya Ukraine imesema vikosi vya Belarus vikiwa na vifaru,magari ya kijeshi na mifumo ya ulinzi wa anga vimeonekana katika eneo la Gomel upande wa Belarus kunakopakana na Ukraine.Soma Pia: Ukraine yaitaka Belarus kuondoa wanajeshi wake mpakani

Kiev imeitaka serikali ya mjini Minsk kutofanya kosa la kuchukuwa hatua yoyote kwa shinikizo la Urusi.

Mashambulizi yaliyofanywa na Urusi nchini Ukraine pia yameifanya Poland na jumuiya ya Nato kujiweka katika hali ya tahadhari upande wa Mashariki mwa Poland.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW