1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yachunguza ikiwa nchi za magharibi zilihusika na uasi

26 Juni 2023

Idara ya intelijensia ya Urusi inachunguza ikiwa idara za ujasusi za nchi za Magharibi zilihusika katika kitisho cha uasi ambao haukufaulu ulioongozwa na wapiganaji wa Wagner siku ya Jumamosi.

https://p.dw.com/p/4T57O
Russland Wirtschaft l Putin hält sich bei einer Veranstaltung den Finger vor den Mund, 2015
Picha: Alexei Nikolsky/Russian presidential press service/TASS/imago

Taarifa hiyo imeripotiwa na shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Urusi TASS ambalo limemnukuu waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov.

Kulingana na ripoti ya shirika la Tass, Lavrov aliyezungumza leo Jumatatu amesema Marekani haikuhusika. Amefafanua kwamba balozi wa Marekani mjini Moscow alitoa ishara kwamba Marekani haikuhusika kwenye tukio hilo la uhaini la kundi la Wagner, na kwamba alitumai kutakuwa na usalama wa zana za nyuklia za Urusi

Lavrov pia alimnukuu balozi huyo wa Marekani akisema uasi huo wa Jumamosi uliofanywa na mamluki wa Wagner ni suala la ndani ya Urusi.

Wito wa mshikamano wa viongozi nyuma ya Putin

Hayo yakijiri, viongozi wa serikali ya Urusi wamesisitiza haja ya mshikamano na rais wao Vladimir Putin.

Waziri Mkuu wa Urusi Mikhail Mishustin, aliyeteuliwa na Putin kusimamia shughuli za baraza la mawaziri, amekiri kuwa Urusi ilikabiliwa na "changamoto dhidi ya utulivu wake". ametoa wito wa utiifu.

Sehemu ya magari ya kijeshi barabarani katika mji wa Rostov-on-Don mnamo Juni 24, 2023, wakati mamluki wa Wagner walipotishia kuelekea Moscow kupindua uongozi wa jeshi la taifa.
Sehemu ya magari ya kijeshi barabarani katika mji wa Rostov-on-Don mnamo Juni 24, 2023, wakati mamluki wa Wagner walipotishia kuelekea Moscow kupindua uongozi wa jeshi la taifa.Picha: Erik Romanenko/ITAR-TASS/IMAGO

"Tunahitaji kufanya kazi pamoja kama timu moja na tuendeleze mshikamano wa vikosi vyote, nyuma ya rais," alisema hayo kwenye mkutano uliotangazwa kwenye vituo vya televisheni vya maafisa wa serikali.

Na kwa mara ya kwanza rais wa Urusi Vladimir Putin ameonekana ambapo ametoa tamko la kwanza tangu uasi huo ulipomalizika. Kupitia tovuti rasmi ya serikali, Putin amewapongeza washiriki wa jukwaa la kiviwanda. Haikubainika mara moja ni wapi kauli hiyo ya Putin iliporekodiwa.

Mnamo Jumamosi, Putin alilihutubia taifa lake akilaani uasi wa kundi la Wagner akisema ni 'kudungwa kisu mgongoni‘ akimaanisha hujuma kwa Urusi. Aliahidi kuliangamiza kundi hilo.

Hata hivyo hajatoa kauli ya hadharani kuhusu makubaliano yaliyofuata yaliyomruhusu kiongozi wa kundi la Wagner, Yevgeny Prigozhin kwenda uhamishoni Belarus, na vilevile yaliyowaruhusu wapiganaji wa Wagner kurejea kambini.

Kiongozi wa kundi la Wagner (Katikati) Jevgeny Prigozhin, alitishia kuongoa wapiganaji wake kuushambula mji mkuu Moscow lakini baadaye alibadili msimamo baada ya makubaliano na rais wa Belarus.
Kiongozi wa kundi la Wagner (Katikati) Jevgeny Prigozhin, alitishia kuongoa wapiganaji wake kuushambula mji mkuu Moscow lakini baadaye alibadili msimamo baada ya makubaliano na rais wa Belarus.Picha: Concord Press Office/ITAR-TASS/IMAGO

Wagner: "Tunaendelea na shughuli katika hali ya kawaida"

Katika tukio jingine, kundi la Wagner limesema linaendelea na shughuli zake katika "hali ya kawaida".

Taarifa hiyo kutoka ofisi ya Wagner imejiri mnamo wakati mustakabali wa kundi hilo ukiwa haujulikani baada ya kitisho chao cha kutaka kupindua uongozi wa jeshi rasmi.

Kwenye taarifa hiyo, ofisi ya Wagner iliyoko mji wa pili kwa ukubwa nchini Urusi Saint Petersburg, imesema licha ya yaliyojiri, kazi inaendelea kama kawaida kulingana na sheria ya shirikisho la Urusi.

Imeongeza kuwa kundi la Wagner limefanya kazi kwa mustakabali wa Urusi na linawashukuru wafuasi wake.

Kiongozi wa kundi hilo, Prigozhin hajaonekana tangu Jumamosi, lakini Urusi imesema atapelekwa katika taifa jirani la Belarus kufuatia makubaliano yaliyoongozwa na Belarus kusitisha uasi wa Wagner.

Apti Alaudinov, kamanda wa vikosi maalum vya Urusi eneo la Akhmat akikagua eneo la mapambano Disemba 20, 2022.
Apti Alaudinov, kamanda wa vikosi maalum vya Urusi eneo la Akhmat akikagua eneo la mapambano Disemba 20, 2022.Picha: Alexander Reka/TASS/IMAGO

Ukraine yakomboa baadhi ya maeneo yaliyochukuliwa na Urusi

Kando na hayo, vikosi vya Ukraine vimekomboa eneo jingine lililochukuliwa na Urusi, ambalo lilikuwa uwanja wa mapambano kati ya majeshi ya pande mbili kusini mwa Ukraine. Hayo ni kulingana na naibu waziri wa Ulinzi wa Ukraine Ganna Malyar

Mwezi huu, Ukraine ilianza mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya vikosi vya Urusi ambavyo vimekamata moja juu ya tano ya nchi yake hususan kusini na mashariki mwa nchi.

Hata hivyo rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amekiri kuwa kasi ya mashambulizi yao ni ya chini na sivyo walivyotarajia, licha ya kuongeza silaha zaidi zikiwemo vifaru walivyopewa na nchi washirika za Magharibi.

(Vyanzo: RTRE, FPE, APE)