1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin aelezea kusikitishwa na kifo cha Daria Dugina

22 Agosti 2022

Idara ya Ujasusi ya Urusi imesema Ukraine inahusika na mauaji ya binti wa mshirika wa karibu wa Rais wa Urusi Vladmir Putin, mwenye misimamo mikali na anatetea uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, Alexander Dugin.

https://p.dw.com/p/4Fsep
Russland Daria Dugina
Daria Dugina, binti wa mshirika wa Rais wa Urusi Vladmir Putin aliyeuawa katika shambulizi la kutegwa kwenye gari Picha: TSARGRAD.TV via REUTERS

Taarifa iliyotolewa Jumatatu na idara hiyo ya FSB na kuripotiwa na mashirika ya habari ya Urusi imeeleza kuwa mhalifu aliyefanya mauaji ya binti huyo, Daria Dugina, ni mwanamke raia wa Ukraine anayefahamika kama Natalia Vovk. Kwa mujibu wa FSB, Vovk alizaliwa mwaka 1979 na jana alikimbilia Estonia, nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Daria, aliuwawa akiwa ndani ya gari aina ya Toyota Land Cruiser baada ya gari hilo kuripuka karibu na kijiji cha Bolshie Vyzyomy kilichoko umbali wa kilomita 40 kutoka kwenye mji wa Moscow. Aidha, Rais Putin ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Daria. Putin amesema tukio la kikatili limeondoa uhai wa Daria, binti mwenye kipaji, mkarimu, mwenye upendo na huruma na muwazi.

Kiev na Kharkiv yazuia sherehe za uhuru

Wakati huo huo, mji mkuu wa Ukraine, Kiev umepiga marufuku sherehe za kuadhimisha uhuru wa nchi hiyo kutoka katika utawala wa Kisovieti zitakazofanyika wiki hii. Sherehe hizo zimepigwa marufuku pia kufanyika katika mji wa Kharkiv kutokana na kitisho kikubwa cha uwezekano wa Urusi kufanya mashambulizi.

Nalo Bunge la Urusi limesema litafanya mkutano maalum kuijadili hali katika kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia kilichoko mashariki mwa Ukraine. Katika taarifa iliyotolewa leo, bunge limesema kikao hicho cha Baraza la Bunge la Urusi, Duma kitafanyika Agosti 25 kujadili kitisho cha usalama katika kinu hicho cha nishati ya nyuklia.

Ukraine-Krieg | Gefechte im Donbass
Wanajeshi wa Ukraine wakiwa katika jimbo la DonetskPicha: Alex Chan Tsz Yuk/SOPA Images/ZUMA Press/picture alliance

Huku hayo yakijiri, Mkuu wa majeshi ya Ukraine Valeriy Zaluzhny amesema takribani wanajeshi 9,000 wa Ukraine wameuawa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine. Zaluzhny amesema watoto wa Ukraine wanahitaji uangalizi maalum kwa sababu baba zao wako kwenye maeneo ya mapambano na pengine miongoni mwao wako mashujaa 9,000 ambao wameuawa. Idadi hiyo ya wanajeshi waliouawa ni ya kwanza kuwahi kutolewa na uongozi wa juu wa jeshi tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, Februari 24.

Ulaya na kuanzishwa mafunzo ya kijeshi

Umoja wa Ulaya utajadili kuanzishwa mafunzo makubwa ya kijeshi kwa vikosi vya Ukraine kwenye mataifa jirani. Mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo, Josep Borell amesema Jumatatu kuwa pendekezo hilo litajasiliwa wiki ijayo katika mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya mjini Prague. Borell amesema ana matumaini pendekezo hilo litaidhinishwa.

Ama kwa upande mwingine, Estonia imetoa wito wa kuchukuliwa hatua za kuiwekea vikwazo vipya Urusi kutokana na uvamizi wake vita nchini Ukraine. Kupitia redio ya nchi hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Estonia, Urmas Reinsalu amesema kuna haja ya kuweka vikwazo vingine zaidi dhidi ya uchukozi wa Urusi kabla ya msimu wa baridi, kwa lengo la kumshinikiza Rais Putin asitishe vita dhidi ya Ukraine.

(AFP, AP, DPA, Reuters)