1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Urusi na Ukraine zashutumiana juu ya kinu cha Zaporizhzhya

5 Julai 2023

Urusi na Ukraine zimetuhumiana kuwa kila upande unapanga kukishambulia kinu kikubwa cha nyuklia cha Zaporizhzhya, kitendo kinachoweza kuzusha janga la kusambaa kwa mionzi ya nyuklia kwenye eneo kubwa barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/4TRY4
Ukraine Saporischschja Region Zerstörung nach Luftangriffen
Picha: Andriy Andriyenko/AP Photo/picture alliance

Urusi na Ukraine zimetuhumiana kuwa kila upande unapanga kukishambulia kinu kikubwa cha nyuklia cha Zaporizhzhya, kitendo kinachoweza kuzusha janga la kusambaa kwa mionzi ya nyuklia kwenye eneo kubwa barani Ulaya.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesema idara za ujajusi za nchi hiyo zimepokea taarifa kuwa jeshi la Urusi limeweka vifaa vinavyofanana na vilipuzi juu ya chemba kadhaa za kufua nishati za kinu cha Zaporizhzhya. Amesema taarifa hizo zinaashiria mpango wa Moscow wa kutaka kukishambulia kinu hicho ambacho ndiyo kikubwa zaidi barani Ulaya.

Wakati huo huo Urusi nayo imetoa tuhuma sawa na hizo ikitahadhirisha kwamba vikosi vya Ukraine huenda vitajaribu kukilenga kinu  cha Zaporizhzhya kwa kutumia makombora au ndege zisizo na rubani kuanzia leo usiku. 

Jumuiya ya Kimataifa imekuwa na mashaka ya uwezekano wa kutokea janga la nyuklia kutokana na makabiliano ya mara kadhaa yaliyoshuhudiwa katika eneo kilipo kinu hicho kinachodhibitiwa na Urusi tangu Machi mwaka jana.