1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na China zajadili mzozo wa Ukraine

30 Machi 2022

Katika vita kati ya Urusi na Ukraine, waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergey Lavrov amefanya mazungumzo hii leo na mwenzake wa China Wang Yi, kuhusu mzozo huo.

https://p.dw.com/p/49DSl
Russland | Innerer Kreis von Putin - Sergey Lavrov
Picha: Russian Foreign Ministry Press Service/AP/picture alliance

Mazungumzo hayo yamefanyika nchini China wakati mamlaka za Ukraine zikiripoti mashambulizi yaliyofanywa na vikosi vya Urusi katika mji wa Chernigiv licha ya ahadi iliyoitoa awali ya kupunguza mashambulizi hayo. 

Soma Zaidi:Marais Joe Biden na Xi Jinping wazungumza kuhusu Ukraine 

China imekuwa ikiiunga mkono Urusi kisiasa kuelekea mzozo huo na imekataa katakata kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ikisema Marekani na mataifa ya magharibi katika ushirika wa kujihami wa NATO ndio hasa chanzo cha mgogoro huo. Mataifa ya magharibi yana wasiwasi kwamba China huenda ikaipatia Urusi msaada wa nyenzo kwenye vita hivyo.

Mwanzoni mwa mazungumzo hayo mapema hii leo katika mji wa Tunxi kusini mashariki mwa China Lavrov alitilia mkazo maslahi ya taifa hilo kupitia mahusiano mazuri baina ya mataifa hayo hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la Urusi, TASS.

"Tuna nia ya kuona uhusiano wetu na Jamhuri ya Watu wa Uchina ukiendelea kukua kwa kasi. Rais wa Shirikisho la Urusi Vladimir Putin na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Xi Jinping walikubaliana kuhusu hili. Leo tutazingatia hatua fulani zinazolenga kuhakikisha kuwa makubaliano yote haya yanatekelezwa," alisema Lavrov.

Kulingana na TASS Lavrov aidha amesema huu ni wakati tete zaidi katika historia ya mahusiano ya kimataifa na kwamba Urusi, China na mataifa mengine yenye nia zinazofanana wanaweza kuimarisha mahusiano ili kuunda mwelekeo mpya wa utangamano duniani.

Ukraine Zerstörung in  Chernihiv
Moja ya jengo katika mji wa Chernihiv nchini Ukraine yaliyoshambuliwa na vikosi vya UrusiPicha: privat

Na huko nchini Ukraine mamlaka zimesema leo kwamba wanajeshi wa Urusi wameushambulia kwa mabomu mji wa Chernigiv ulioko kaskazini mwa nchi hiyo licha ya ahadi ya Urusi iliyoitoa awali kwamba ingepunguza shughuli za kijeshi katika eneo hilo. Gavana wa Chernigiv, Vyacheslav Chaus ameandika kwenye mitandao ya kijamii na hapa nanukuu "adui amepunguza shughuli zake kwa kuishambulia Nizhyn, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya angani, usiku mzima wa jana." Tamko hilo liliungwa mkono na mshauri wa rais wa Ukraine, Oleksiy Arestovych.

Soma Zaidi: Urusi kupunguza operesheni za kijeshi karibu na Kyiv

Arestovych aidha, amesema kupitia hotuba ya televisheni kwamba jeshi la Urusi limerejesha baadhi ya wanajeshi wake mashariki mwa nchi hiyo. Amesema Urusi imewahamishia baadhi ya wanajeshi kutoka maeneo ya karibu na mji mkuu Kyiv katika juhudi zake za kuwazingira wanajeshi wa Ukraine ili wasiweze kusogelea maeneo mengine.

Nje ya Ukraine, Ujerumani imeanzisha mpango wa dharura wa kusimamia usambazaji wa gesi nchini humo hatua ambayo haijashuhudiwa kabla huku waziri wa masuala ya uchumi Robert Habeck akiyatolea mwito makampuni na watu binafsi kujaribu kupunguza matumizi ya nishati kadri inavyowezekana wakati taifa hilo tajiri zaidi barani Ulaya likijaribu kujiondoa kwenye utegemezi wa gesi kutoka Urusi ambayo inasisitiza manunuzi kufanyika kwa sarafu yake badala ya Euro iliyotumika awali.

Soma Zaidi: Ulaya haitonunua gesi ya Urusi kwa sarafu ya taifa hilo

Mashirika: DPAE/APE/DW