1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wapinga marufuku ya simu za mikononi vituoni

Emmanuel Lubega16 Februari 2016

Amama Mbabazi pamoja na Kiza Besigye wanasema amri hiyo ya Tume ya Uchaguzi ni hatua ya kwanza ya kutoa taarifa za kupotosha kuhusu matokeo ya uchaguzi, huku wakizuia taarifa za mara kwa mara na sahihi.

https://p.dw.com/p/1Hw5p
Mgombea urais Amama Mbabazi.
Mgombea urais Amama Mbabazi.Picha: DW/E. Lubega

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi, Badru Kigunddu, aliagiza kwamba simu za mkononi hazitaruhusiwa katika umbali wa mita 100 kutoka kituo cha kupigia kura. Umbali huu ni sawa na upande mmoja wa uwanja wa mpira hadi mwingine.

Lakini wagombea urais wamepinga vikali agizo hilo wakielezea kuwa ndiyo hatua mojawapo inayopelekea wizi wa kura. Wakiwahutubia wandishi habari kwenye makaazi yao binafsi, Kasangati na taa wa Kololo, Besigye na Mbabazi walishtumu Tume hiyo kwa "kuendelea kupokea mashinikizo kutoka kwa utawala wa NRM."

Aidha wagombea hao, ambao wako kwenye duru ya mwisho wa kampeni zao, walipinga matumizi ya makundi ya wazuiaji uhalifu ambao walisajiwa na polisi.

Akiwa kwenye kikao kikao kingine, mkuu wa ujumbe wa waangalizi kutoka Umoja wa Ulaya, Eduard Kukan, alisita kutoa kauli kuhusu agizo la kupiga marufuku simu za mkononi, lakini alikubaliana na kero hiyo ya wagombea kuhusu kutumiwa kwa wazuiaji uhalifu katika uchaguzi utakaofanyika Februari 18.

Kulingana na takwimu za uchaguzi wa mwaka 2011, asilimia 42 ya waliosajiliwa kupiga kura wapatao milioni 5.6 hawakufanya hivyo. Rais Museveni alipata kura milioni 5.2 katika uchaguzi huo na kwa mtazamo wa Mbabazi iwapo idadi kubwa haitapiga kura basi kiongozi wa sasa atapata ushindi ambao hastahili. "Hatua zozote za kusababisha hofu miongoni mwa wapigaji kura ni hila nyingine kuwazuia kupiga kura."

Leo ndio siku ya mwisho ya kampeni na wagombea wakuu kwa nafasi ya rais wanaendesha kampeni zao jijini Kampala.

Hapo jana, Besigye hakuweza kuzindua kampeni zake baada ya wafuasi wake kuokabiliana na polisi. Jumla ya watu 19, akiwemo askari wa polisi mwanamke, walijeruhiwa huku washukiwa 22 wakikamatwa kwa kuhusika katika ghasia zilizokikumba kituo cha biashara cha Wandegeya jirani na Chuo Kikuu cha Makerere, ambapo Besigye alipanga kufanya mkutano wake.

Mwandishi: Lubega Emmanuel/DW Kampala
Mhariri: Mohammed Khelef