1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani nchini Burundi washinda katika uchaguzi wa kidemokrasia

Epiphania Buzizi10 Juni 2005

Chama cha waasi wa zamani wa kihutu nchini Burundi cha FDD, kimejinyakulia ushindi katika uchaguzi wa madiwani.

https://p.dw.com/p/CEFo
Zoezi la upigaji kura nchini Burundi
Zoezi la upigaji kura nchini BurundiPicha: AP

Uchaguzi huo wa kwanza kufanyika nchini humo chini ya mfumo wa vyama vingi katika kipindi cha miaka 12,unaandaa mwingine wa wabunge na wa urais, utakaofanyika baadae mwezi wa Agosti mwaka huu.

Tume huru ya uchaguzi nchini Burundi imetangaza kwamba chama cha FDD kimepata ushindi kwa asilimia 55 katika mabaraza ya uchaguzi 1,781 kati ya jumla ya mabaraza 3,225 ya kupigia kura, katika uchaguzi wa madiwani ulipofanyika Ijumaa iliyopita.

Chama tawala cha FRODEBU, kimefuata kikiwa kimepata uungwaji mkono katika maeneo ya uchaguzi 820, nacho chama cha UPRONA kimepata nafasi ya tatu kikiwa na uungwaji mkono katika mabaraza 259 ya uchaguzi,huku chama cha CNDD, ambacho ni mkondo wa FDD,kikijipatia viti 134. Mabaraza mengine yamechukuliwa na vyama vidogo vilivyosalia.

Uchaguzi huo unaandaa mwingine wa wabunge na wa urais, ambao utafanyika mwezi Agosti mwaka huu kwa lengo la kuimarisha demokrasia nchini Burundi, baada ya machafuko ya kikabila yaliyodumu kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi nchini Burundi, Paul Ngarambe, amesema uchaguzi wa Burundi ni hatua muhimu katika juhudi za amani nchini humo.

Ameongeza kusema kuwa, matokeo ya uchaguzi huo yanaweza kubadilika katika siku zijazo kutegemeana na malalamiko yatakayotolewa ,lakini kuna matarajio makubwa kwamba mataokeo hayo yatabaki yalivyo kwa sasa.

Na haya yakiarifiwa, msemaji wa chama cha FRODEBU Jean Dedieu Mutabazi, alisema jana kwamba chama chake kinapinga matokeo hayo,akisema kuwa chama cha FDD kilitoa vitisho vya kuwaua wapiga kura ikiwa wangewapigia kura wafuasi wa vyama vingine.

Msemaji wa chama hicho, amesema FRODEBU itapeleka mashtaka mahakamani kudai uchaguzi huo urudiwe.Uchaguzi wa madiwani nchini Burundi ulionekana kama mtihani wa kupima uimara wa vyama vya kisiasa vipatavyo 30, kutoka kabila la wahutu na watutsi ambao kwa pamoja wamewania nafasi bungeni.

Wadadisi wa mambo wanasema, matokeo ya uchaguzi huo ni muhimu katika kuamua muundo wa bunge la Burundi, ambalo ndilo litakalomchagua rais wa nchi hiyo.

Maafisa wa uchaguzi wa madiwani wamesema asilimia kati ya 70 na 80 ya watu milioni 3 waliojiandikisha kupiga kura, walishiriki katika uchaguzi huo.

Chama cha waasi wa zamani cha FDD kilishiriki katika serikali ya mpito nchini Burundi mwaka 2003,na kujenga matumaini ya kupatikana kwa amani nchini humo, baada ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kuzuka nchini Burundi mwaka 1993.

Watu wapatao laki 3 waliuawa katika mauaji hayo, yaliyoendeshwa na wahutu dhidi ya kabila dogo la watutsi ambalo kwa muda mrefu lilishika madaraka nchini Burundi.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa nchini humo wanasema ushindi wa chama cha FDD haushangazi ,na huenda chama hicho kikajinyakulia ushindi hata katika uchaguzi wa wabunge.

Wakati haya yakiarifiwa,mazungumzo ya amani yaliyokuwa yamaepangwa kufanyika mjini Dar es Salama,kati ya serikali ya Burundi na chama cha waasi kilichosalia cha FNL Perpehutu ,yamecheleweshwa baada ya wajumbe wa waasi hao kushindwa kuhudhuria.Mazungumzo hayo yalipangwa kufanyika siku ya Jamatano.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na afisa mmoja wa serikali ya Tanzania,rais wa Burundi Domitien Ndayizeye amekwisha wasili mjini Dar es Salama, lakini upande wa waasi wa FNL haujatuma wajumbe wao.

Rais wa Burundi Ndayizeye na kiongozi wa FNL Agaton Rwasa, walitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano tarehe 15 mwezi Mei ,na kukubaliana kuunda kamati ya kiufundi katika kipindi cha mwezi mmoja ,ambayo jukumu lake ni kuweka mpango wa kutekeleza makubaliano hayo ya kusitisha mapigano.

Lakini licha ya makubaliano hayo,waasi hao wamekuwa wakilaumiwa kwa kuendesha mashambulizi ya hapa na pale,na wamelaumiwa kuvuruga uchaguzi wa madiwani uliofanyika nchini Burundi wiki iliyopita.

Mashambulizi ya makombora yariripotiwa kuendeshwa katika maeneo ya Bujumbura vijijini siku ya uchaguzi na kupelekea uchaguzi kurudiwa kwenye wilaya sita mapema wiki hii.