1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Belarus wafanya maandamano ya mwishoni mwa juma

Sekione Kitojo
15 Agosti 2020

Upinzani nchini Belarus umejitayarisha  na  maandamano  mapya mwishoni mwa juma leo Jumamosi wakati mbinyo ukiongezeka dhidi ya kiongozi huyo mbabe Alexander Lukashenko kutoka  mitaani na  viongozi  wa Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/3h0rj
Polen Krakau Solidaritätsproteste mit Belarus
Picha: picture-alliance/NurPhoto/B. Zawrzel

Wakati upinzani ukiendelea  kupata  nguvu  baada  ya  siku kadhaa  za maandamano  kuhusiana  na uchaguzi wa  rais  unaobishaniwa  uliofanyika Jumapili  iliyopita , mgombea  mkuu wa upinzani  katika  uchaguzi  huo Svetlana Tikhanovskaya amewataka  waungaji wake  mkono  kufanya maandamano tena  mwishoni mwa  juma  hili.

Belarus Wahl 2020 | Baranovichi
Maandamano ya mwishoni mwa juma mjini Minsk kupinga matokeo ya uchaguzi wa BelarusPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Grits

Wamekusanyika  mchana  siku  ya  Jumamosi karibu na  kituo kikuu  cha treni  cha Pushkinskaya  katika  mji  mkuu  Minsk kwa kumuenzi Alexander Taraikovsky , muandamanaji  mwenye  umri  wa  miaka 34 ambaye  alifariki hapo siku  ya  Jumatatu  na  ambaye  mazishi  yake  yanafanyika.

"Maandamano  kwa  ajili  ya  uhuru" yamepangwa kufanyika  katikati ya Minsk kesho  Jumapili, wiki  moja  baada  ya  uchaguzi  huo  unaobishaniwa kwamba  Lukashenko  mwenye  umri  wa  miaka  65 anadai  kuwa ameshinda  kwa  asilimia  80  ya  kura.

Tikhanovskaya , mwenye  umri  wa  miaka  37 ambaye ndio  kwanza amejiingiza  katika  siasa  na  ambaye  aligombea  baada  ya  wagombea wengine  wa  upinzani  pamoja  na mume  wake  kufungwa, anamshutumu Lukashenko kwa kughushi  kura na  anadai  ajiuzulu ili  uchaguzi  mpya uweze  kufanyika.

Polen Krakau Solidaritätsproteste mit Belarus
Muandamanaji mjini Minsk akishikilia bango lenye picha ya kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko ikiwa na damu.Picha: picture-alliance/NurPhoto/B. Zawrzel

Aikimbia nchi

Ameikimbia  nchi  hiyo siku  ya  Jumanne na  kukimbilia  nchi  jirani  ya Lithuania, akiwa  pamoja, washirika  wake  wakisema  amekuwa  katika shinikizo  kutoka kwa maafisa wa  serikali, lakini  siku  ya  Ijumaa  alijitokeza akitoa  wito wa  kufanyika  maandamano  mwishoni  mwa  juma, "ya mkusanyiko  wa  amani" katika  miji  nchini  kote.

Pia  anataka  maafisa  wawajibike  kutokana  na  ukandamizaji  wa  polisi dhidi ya  waandamanaji  baada  ya  uchaguzi  ambapo ukandamizaji  huo umeshuhudia  zaidi  ya  watu 6,700 wakikamatwa.

Polisi  wametumia  risasi za  mipira, mabomu  ya  kusitua na takriban katika tukio  moja, risasi  za  moto  zilitumika  kuyatawanya makundi, ambapo mamia walijeruhiwa.

Maafisa  wamethibitisha vifo viwili katika machafuko  hayo, ikiwa ni  pamoja na Taraikovsky  ambae wanasema  alifariki  wakati kiripuzi kiliporipuka mkononi mwake wakati wa  maandamano, na mtu mwingine  aliyefariki akiwa  mikononi mwa  polisi  baada  ya  kukamatwa  katika  mji  wa  kusini  mashariki  wa Gomel.

Belarus Wahlen Polizeigewalt | Proteste in Minsk
Polisi wakimpiga muandamanaji mjini MinskPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Grits

Waachiwa  huru

Siku  ya  Ijumaa maafisa  walianza kuwaachia  mamia  ya watu waliowakamata na wengi walitoka  kutoka  kizuwizini wakielezea madhila makubwa ya kupigwa na  kuteswa.

Shirika  la  kutetea  haki  za  binadamu  Amnesty International limeshutumu, kile  ilichoeleza  kuwa  ni "kampeni wa mateso  nchini  nzima pamoja  na matendo  mengine  ya  ukiukaji haki yanayofanywa  na  mafisa  wa  Belarus ambao wana nia  ya  kuzima maandamano  ya  amani  kwa  njia  yoyote ile."

Situation in Minsk Belarus
Mwanamke akiweka maua katika eneo alilouwawa Alexander Taraikovsky mjini MinskPicha: picture-alliance/dpa/V. Sharifulin

Kiongozi  wa  Belarus Alexander Lukashenko  amesema  leo Jumamosi (15.08.2020) anataka  kuzungumza  na  kiongozi  wa  Urusi Vladimir Putin wakati  maandamano  nchini  mwake yakiongezeka  kuhusiana  na  uchaguzi ambao unabishaniwa. "Mapambano  dhidi  ya  Belarus  yanaongezeka. Tunahitaji  kuwa  na  mawasiliano  na  Putin, rais wa  Urusi , ili  niweze kuzungumza  nae sasa," Lukashenko alisema  katika  mkutano  na  maafisa wa  serikali. "Kwasababu hii tayari ni  kitisho sio tu kwa  Belarus."