1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNICEF: Zaidi ya watoto 40,000 wako hatarini Raqqa

9 Juni 2017

Shirika la Kimataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeonya kwamba mapigano ya kuukomboa mji wa Raqqa yanatishia kugharimu maisha ya zaidi ya watoto 40,000 katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/2eQPI
Syrien Krieg - Kind in Rakka
Picha: picture-alliance/AP Photo/Jonathan Hyams, Save the Children

Shirika la Kimataifa la kuwahudumia watoto, UNICEF limeonya kwamba mapigano ya kuukomboa mji wa Raqqa ambao ni ngome ya wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS ulioko Kaskazini mwa Syria yanatishia kugharimu maisha ya zaidi ya watoto 40,000, katika eneo hilo. 

Taarifa iliyotolewa leo hii inasema machafuko hayo yamesababisha idadi kubwa ya watu kutoka ndani na nje ya mji huo kuyakimbia makazi yao, huku kiasi ya watoto 80,000 hivi sasa wakiwa wameyahama makazi yao na kuishi katika makazi ya muda na makambi.  

Majeshi ya Syria yanayoungwa mkono na Marekani yalianzisha mashambulizi katika mji wa Raqqa mapema wiki hii na mashambulizi ya anga ya muungano wa majeshi unaoongozwa na Marekani yameongezeka. 

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Sarikis Kassargian anasema, wana imani kubwa kwamba Marekani inahusika kwa kiasi kikubwa katika kufikiwa maamuzi hayo ya kuanzisha mashambulizi.

"Siamini kulikuwa na makubaliano kuhusu Raqqa na Marekani na Urusi. Zaidi ya hilo ninadhani Raqqa ni tatizo katika mahusiano ya Urusi na Marekani kwa upande mmoja na kati ya Urusi na Uturuki kwa upande mwingine. Lakini inaonekana kwamba Donald Trump pia anasisitiza mabadiliko mapya katika eneo hili. Na ndio maana amelishinikiza jeshi la Syria kuanza mashambulizi kuukomboa mji wa Raqqa, amesema mchambuzi huyo.

"Kiasi ya watoto 40,000 katika mji wa Raqqa wanakabiliwa na hatari kubwa. Wengi hukutwa na dhahama katikati ya mashambulizi" amesema Mkurugenzi mkazi wa UNICEF Geert Cappelaere, huku akitaka kuandaliwa kwa njia salama za kupita raia wanaotaka kutoka kwenye mji huo.

Syrien Belagerung Stadt Douma
Watoto katika mji wa Raqqa hukumbwa na dhahama katikati ya mapiganoPicha: DW/F. Abdullah

Wakati mapigano hayo yakizidi kushika kasi katika mji wa Raqqa na viunga vyake, shirika hilo la UNICEF linaangazia pia namna ya kufikisha mahitaji kwa familia zilizo katika mazingira magumu kwa kupeleka lita 975,000 za maji kila siku kwa watu 1,200 walioyahama makazi yao.

UNICEF imesema, tangu mwezi Novemba 2016, mapigano yasiyokuwa na huruma kwa raia katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Raqqa yamesababisha watu 107,000 kuhama makazi. Kuongezeka kwa mashambulizi kumesababisha uharibifu wa miundombinu na kuwatawanya raia, na familia zinatafuta mahala salama pa kuishi, katika makazi duni ya muda na makambi kwenye eneo ambalo upatikanaji wa huduma muhimu ni mgumu.

Mapema siku ya jana, Umoja wa Mataifa ulielezea masikitiko yake kuhusu hali ya usalama na ulinzi kwa raia waishio ndani ya mji huo unaodhibitiwa na kundi la Dola la Kiislamu, IS, wa Raqqa nchini Syria wakati mapigano katika mji huo yakizidi kushika kasi. 

Linda Thom kutoka ofisi za Umoja wa Mataifa zinazoratibu misaada ya kibinaadamu ameliambia shirika la habari la dpa kwamba katika siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa dalili zinazotishia kuongezeka kwa idadi ya vifo na majeruhi kutokana na mashambulizi ya anga, pamoja na uharibifu wa miundombinu ya raia.

Mashambulizi ya anga katika mji wa Raqqa yaliyofanywa kati ya Juni 5 hadi 7 yamesababisha vifo vya watu 9 na kuharibu miundombinu  na majengo  ikiwemo benki, shule mbili na msikiti.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman