1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNHCR yafanya ziara katika kambi za wakimbizi Uganda

Lubega Emmanuel10 Machi 2021

Mkuu wa shirika la UNHCR Fillipo Grandi ameonya kuwa maisha yatazidi kuwa magumu kwa wakimbizi nchini Uganda wakati mashirika na mataifa wafadhili yakitanguliza misaada kwa raia wao walioathiriwa na COVID-19

https://p.dw.com/p/3qRRc
Uganda UNHCR-Flüchtlingslager
Picha: picture-alliance/dpa/Belga/B. Doppagne

Hayo ameyasema baada ya kuzuru kambi za wakimbizi kaskazini mwa Uganda jana 09.03.2021.  

Ziara ya mkuu wa shirika la UNHCR linalowashughulikia wakimbizi Fillipo Grandi imekuwa ya kushtukiza nchini Uganda pale alipokosa kupokelewa rasmi na mawaziri wanaohusika moja kwa moja na masuala ya wakimbizi kama ilivyo ada.

Mwenyewe amefafanua kuwa alitaka kuja kujionea kwa macho yake hali ngumu inayowakumba wakimbizi hasa katika kambi ya Bidibidi wilayani Yumbe Kaskazini mwa nchi hiyo ambayo imetoa mastakimu kwa wakimbizi zaidi ya miliono moja laki nne. 

"Wakimbizi wamekumbwa na matatizo makubwa ya mahitaji na si tu nchini Uganda lakini pia katika mataifa ya Afrika mashariki na mojawapo imekuwa kupunguzwa kwa chakula wanachopewa," amesema.

Grandi amezuru shule, vituo vya afya, vyanzo vya maji na makazi ya wakimbizi kutathimini jinsi huduma za kijamii zilivyoathirika kufuatia janga la COVID-19.

Viongozi wa serikali ya Uganda sehemu hiyo wamelalamikia kiwango cha juu cha uharibifu wa mazingira kwani idadi hiyo kubwa ya wakimbizi wapatao laki mbili thelathini na tano elfu inategemea nishati ya kuni na mkaa. Mkuu wa wilaya ya Yumbe Caroline Angolere ametamka hivi akiwahutubia waandishi habari.

"Kutokana na idadi kubwa ya watu, mazingira yameharibiwa kutokana na uchomaji mkaa kama njia ya kuingiza kipato kwa baadhi lakini pia kwa ajili ya nishati."

Wito wa misaada zaidi watolewa

Uganda Flüchtlinge aus DR Kongo UNHCR Camp
Raia wa DRC waliokimbia mapigano nchini humo wakiwa katika kambi ya wakimbizi ya Kyangwali, Uganda. Picha: Reuters/J. Akena

Mkuu wa UNHCR amewahimiza wakimbizi kuzidisha juhudi katika kazi za kuingiza kipato pamoja na kuzalisha chakula chao kwenye mashamba waliyopewa na serikali ya Uganda. Kwa namna hii, wakimbizi hao ambao wengi ni raia wa Sudan Kusini na hawajui hali ya amani itarejea lini nchini kwao wataweza kuchangia katika kukidhi mahitaji yao msingi badala ya kusubiri misaada ambayo inazidi kwa adimu.

Lakini pia ametoa mwito kwa jamii ya wahisani kutoa misaada ambayo itawawezesha wakimbizi na wenyeji wao kuboresha maisha yao wakishiriki katika shughuli endelevu za kujikimu mahitaji yao.

"Mwaka huu nadhani hali itakuwa ngumu zaidi kwani hata katika mataifa wa hisani kuna changamoto za kiuchumi na ndo maana tungependa wakimbizi wasaidiwe kuzalisha chakula chao wenyewe ndio sababu ya ziara yangu."

Akikamilisha ziara yake ya siku tatu Uganda, Fillipo Grandi amekutana na rais Yoweri Museveni kushauriana kuhusu njia za kuwapunguzia wakimbizi makali ya maisha katika kipindi ambapo misaada imepungua pakubwa.