1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNHCR imepata kamishana mpya

Lillian Urio15 Juni 2005

Antonio Guterres, aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Ureno, ndio kamishana mpya wa shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR. Bwana Guterres ataongoza shirika hilo, lenye makao makuu Geneva nchini Uswisi, kwa kipindi cha miaka mitatu.

https://p.dw.com/p/CHgU
Antonio Guterres, Kamishna mpya wa UNHCR
Antonio Guterres, Kamishna mpya wa UNHCRPicha: dpa

Kazi ya kuiongoza shirika linalo hudumia wakimbizi, la UNHCR, inaonekama kama ndio kazi ngumu zaidi kuliko kuongoza mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa. Akiwa kama kiongozi wa UNHCR, Bwana Guterres, mwenye umri wa miaka 56, atatakiwa kuwahudumia watu milioni 17, wakiwemo wakimbizi wa kivita, siasa na maafa ya asili.

Kwa sasa mojawapo ya kisa kinacho ishughulisha shirika hili ni tatizo la Darfur, huko Sudan. Kwa makadirio ya Umoja wa Mataifa, watu milioni moja wanahitaji misaada ya chakula, mahema na huduma za afya. Lakini kutokuwepo na usalama kunapelekea wale wanaotakiwa kutoa misaada, kuwa mashahidi wa janga.

Kabla ya siku ya kazi kuanza rasmi, ambayo ni tarehe 5 mwezi huu, Bwana Guterres alienda kwenye makao makuu ya UNHCR, huko Geneva, na kujitambulisha kwa wafanyakazi. Alienda baada tu ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wenye mamlaka ya kuidhinisha, kukubaliwa kwake. Bwana Guterres ni mtu mwenye umbo dogo na anaonekana kama ni mtu aliyerahisi kukubalika.

“Tafadhali msiogope kuniambia ukweli, hata kama sio wa kufurahisha na hata kama nikisahau nilichosema hapa leo.”

Bwana Guterres alisema kwa utani katika ukumbi wa jengo la UNHCR, lakini aliendelea kwa kujieleza:

“Kwangu mimi ni heshima kuwepo hapa mbele yenu na itakuwa heshima kubwa zaidi kujiunga na nyie. Watu mnao jituma, wenye uwezo mkubwa na ushujaa kuliko wengine wote katika mashirika ya kimataifa. Wakati mwingine mnafanya kazi katika mazingira magumu sana.”

Jambo la Bwana Guterres kujaribu kwa kila njia kujenga uhusiano mzuri na wafanyakazi wake wapatao 6000, linatokana na tabia yake ya kufanya kazi katika ushirikiano. Ni mtu mwenye sifa za huruma na kupendwa. Sifa ambazo, mwaka 1996, zilimpelekea kuwa Waziri Mkuu wa Ureno.

Kamishna huyu mpya pia anajaribu kujenga uhusiano kwa sababu ya tatizo la imani kutokuwepo ndani ya UNHCR. Aliyemtangulia kamishna wa zamani wa shirika hilo, Ruud Lubbers alijiuzulu, mwanzo wa mwaka huu, kutokana na tuhuma za kumdhalilisha mtu kijinsia. Uamuzi ambao hadi leo unapingwa.

Lakini hamna mtu mwenye mashaka na uwezo wa mwanasiasa huyu wa Kireno kufanya kazi hii. Hata kama alishindwa vibaya katika awamu ya pili ya uongozi wake huko Ureno, lakini analeta ujuzi wa kutosha katika jumuiya ya kimataifa.

Alipata sifa nzuri wakati wa kipindi chake cha Urais wa Umoja wa Ulaya, jinsi alivyoshughulikia suala la Austria, pale chama cha ubaguzi kipoingia madarakani. Hadi sasa alikuwa kiongozi wa socialist Kimataifa na inaaminika kwamba kutokana na yeye kujuana na watu wengi itamsaidia katika kazi hii mpya. Mwenyewe anaeleza kwanini amekubali kazi hii:

"Niko hapa na imani, unyenyekevu na shauku. Imani sababu nina amini malengo makuu ya kazi hii na nitakuwa na jitihada ili yatimizwe duniani kote. Unyenyekevu sababu nina mengi ya kujifunza. Na shauku sababu sidhani kama ningeweza kuchagua kazi muhimu nyingine, inayozidi hii, na kuipigania”.

Kutoa msaada wa watu miluioni 17, duniani kote, na kuwatetea, hiyo ndio kazi ya UNHCR, iliyoundwa miaka 50 iliyopita.