1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Unachopaswa kufahamu kuhusu uchaguzi wa Marekani

3 Novemba 2020

Wakati wamarekani wanapiga kura leo hii kumchagua rais kati ya wagombea wa vyama kuu viwili, Donald Trump wa Republican na Joe Biden wa chama cha Democratic, dunia inasubiri kwa hamu kuona nani ataibuka mshindi.

https://p.dw.com/p/3kngL
USA Präsidentschaftswahl 2020
Picha: Go Nakamura/Reuters

Uchaguzi unaoendelea leo nchini Marekani umevunja rekodi kwa idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura mpaka sasa. Hii imetokana na janga la virusi vya corona iliyosababisha baadhi ya sheria za upigaji kura kubadilika. Kwa sasa watu wameweza kupiga kura za mapema kabla ya siku ya uchaguzi na pia kumekuwa na uwezekano wa kupiga kura kwa njia ya posta. Mpaka sasa tayari wamarekani karibu milioni 100 wameshapiga kura. Kwa jimbo la Texas pekee idadi ya watu waliopiga kura za mapema walizidi jumla ya watu waliopiga kura katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2016. Kutokana na hilo, idadi ya wapiga kura katika uchaguzi huu inategemewa kuvunja rekodi.

Ukiachilia upigwaji huo wa kura za mapema kutokana na janga la virusi vya corona, wapiga kura waliojitokeza siku yenyewe ya leo ya uchaguzi pia wanategemewa kuwa na umuhimu mkubwa. Wanachama wa chama cha Republican walipendelea upigaji kura wa moja kwa moja, kwahiyo Rais wa sasa Donald Trump anakadiria kwamba waungaji wake mkono watajitokeza kwa wingi leo Jumanne. Kwa upande wa Democrats upigaji kura wa mapema ni kama umewasaidia wao, lakini bado wapiga kura wenye asili ya Afrika, ambao hupigia chama hicho kura kwa wingi, wao wanaopendelea kupiga kura za moja kwa moja. Hiyo inamaanisha kujitokeza kwao katika uchaguzi wa leo kunaweza kuwa na manufaa kwa mgombe wa chama cha Democrat Joe Biden. 

USA Lumberton North Carolina | Wahlkampf Präsident Trump
Rais Trump wa Republican anatafuta muhula wa piliPicha: Jason Moore/Zuma/imago images

Rais wa Marekani hategemewi kuchaguliwa na kura za raia tu, bali ushindi wake hutegemea pia mfumo wa uchaguzi kupitia wajumbe wa majimbo au electoral college. Mshindi wa Urasi inabidi apate kura takribani 270 kutoka kwa wajumbe hao 538 kutoka majimbo mbali mbali ili kushinda uchaguzi.

Kati ya majimbo yenye idadi kubwa ya kura za wajumbe hao ni kama vile jimbo la Texas lenye kura 38, Florida lenye kura 29 na Pennsylvania lenye kura 20.

Kwa kawaida matokea ya mshindi wa uchaguzi hutoka masaa sita baada ya vituo vya kupiga kura kufungwa, lakini katika uchaguzi wa mwaka huu uliojumuisha upigaji kura wa njia ya posta, unaweza kusababisha matokeo ya mshindi kuchelewa kutolewa. Baadhi ya majimbo yalianza kuhesabu kura kabla ya siku ya uchaguzi, wakati majimbo mengine hayakuruhusiwa kufanya hivyo na kuanza kuhesabu kura hizo siku ya leo baada ya uchaguzi.  Majimbo mengine yameacha watu waendelee kurudisha kura zao katika siku chache zinazofuata.

US Wahl 2020  Joe Biden  Rally
Mgombea wa Democratic BidenPicha: Alexandra Wimley/picture alliance/AP Photo

Kama ikitokea katika majimbo maalum hama mgombea uraisi aliyepata idadi ya kura zaidi ya 270 zinazotokana na mfumo wa uchaguzi kupitia wajumbe wa majimbo, hiyo inamaanisha mshindi atajulikana katika siku au wiki zijazo mpaka kura zilizotumwa kwa njia ya posta zihesabiwe zote. Kama kutakuwa na ushindi mwembamba sana kutakuwa na michakato ya kisheria itakayobidi kufuatwa mpaka kufikia tarehe 8 Disemba ili kuweza kumpata mshindi.

Ukiachilia kupiga kura kwa ajili ya Uraisi, wamarekani pia hupiga kura kuchagua wabunge wa congress. Wabunge wa viti takribani 435 katika baraza la seneti na baraza la wawakilishi pia huchaguliwa katika uchaguzi. 

Viti takribani 35 katika maeneo yanayoongozwa na chama cha Republican yapo katika uchaguzi wa baraza la seneti na Wademocrat wanahitaji kuongeza viti vinne tu, ili kuweza kuongoza baraza la seneti.

Mwandishi: Harrison Mwilima