1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaupinga mpango wa Israeli

20 Desemba 2012

Katika hali isiyotarajiwa na nadra kuchukuliwa, wanachama 14 kati ya 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wametoa kauli za kupinga mipango ya Israeli ya kujenga makaazi mapya ya wayahudi, Jerusalem Mashariki.

https://p.dw.com/p/1761X
Wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama la UN
Wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: dapd

Kauli hiyo wameitoa baada ya Marekani kuzuia jaribio la Israeli kuchukuliwa hatua kali kutokana na hatua yake hiyo. Balozi wa India kwenye Umoja wa Mataifa, Hardeep Singh Puri ameelezea kauli nne tofauti zilizotolewa na wanachana wanane wasiofungamana na upande wowote, wanachama wanne wa Ulaya, Urusi na China kama mpango wa pili wa kuishutumu mipango ya Israeli baada ya kufahamika wazi kuna uwezekano wa Marekani kutaka kupiga kura ya turufu kuhusu suala hilo. Marekani, ndiye mwachama pekee wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo haijalaani mipango hiyo ya Israeli. Kauli zote hizo zimetolewa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, baada ya baraza la usalama la umoja huo kuielezea hali hiyo ya Mashariki ya Kati.

Marekani haikutoa kauli yoyote katika mkutano huo. Marekani ambayo kwa kawaida imekuwa mlinzi mkubwa wa Israeli katika baraza la usalama, ilizuia azimio la Februari mwaka uliopita lililokuwa linalaani vikali ujenzi wa makaazi unaofanywa na Israeli. Mwanachama yeyote wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na China, zinaweza kupiga kura ya turufu katika azimio hilo. Alipoulizwa kuhusu taarifa iliyopangwa na wajumbe wa baraza hilo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani, Victoria Nuland alisema kila nchi ni lazima ionyeshe uwakilishi wake na hiyo ndiyo njia inayoendelea.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani, Victoria Nuland
Msemaji wa wizara ya nje ya Marekani, Victoria NulandPicha: Getty Images

Ban Ki-Moon aitolea wito Israeli

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amesema Israeli inachukua mkondo wa hatari ambao utaathiri kupatikana kwa amani. Ameitaka Israeli kuachana na mpango wake huo ambao unaonekana kuhatarisha amani ya Mashariki ya Kati. Jana Jumatano, Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu alisema kuwa serikali yake itaendeleza ujenzi wa makaazi ya Wayahudi kuzunguka Jerusalem Mashariki, licha ya ukosoaji huo wa mataifa ya Magharibi. Hata hivyo, Nuland alisema Marekani imesikitishwa sana na Israeli kusisitiza kuendelea na mpango wake na kwamba unaliweka hatarini lengo la kupatikana suluhisho la mataifa mawili.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilianza tena mazungumzo kuhusu azimio la kulaani ujenzi wa makaazi ya walowezi baada ya mwezi uliopita Israeli kutangaza itajenga nyumba 3,000 katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, maeneo ambayo Wapalestina inayataka kama taifa lao la baadae pamoja na Gaza. Lakini wanadiplomasia wamesema inaonekana kuwa Marekani haiko tayari kuliunga mkono azimio hilo. Inakadiriwa kuwa Waisraeli 500,000 na Wapalestina milioni 2.5 wanaishi katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki. Israeli iliitangaza hatua hiyo siku moja baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuipandisha hadhi Palestina na kuwa kama taifa mwangalizi lisilo mwanachama katika Umoja wa Mataifa.

GettyImages 152748732 UN Secretary-General Ban Ki-Moon addresses the 67th UN General Assembly at the United Nations headquarters in New York, September 25, 2012. AFP PHOTO/Emmanuel DUNAND (Photo credit should read EMMANUEL DUNAND/AFP/GettyImages)
Katibu Mkuu wa UN Ban Ki-moonPicha: Getty Images

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE
Mhariri: Sekione Kitojo