1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaunga mkono pendekezo la AU kuongeza vikosi Somalia

Admin.WagnerD22 Oktoba 2010

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeunga mkono pendekezo la Umoja wa Afrika la kuongeza walinda amani nchini Somalia, lakini linautaka kwanza Umoja wa Afrika kutoa maelezo ya kina kuhusu mpango huo.

https://p.dw.com/p/Pl2E
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moonPicha: AP

Umoja wa Afrika unataka kuongeza kikosi chake cha walinda amani nchini Somalia, kijuilikanacho kama AMISOM, kutoka wanajeshi 7, 200 waliopo sasa hadi 20,000. Unataka pia kutenga eneo ambalo ndege haziruhusiwi kuruka na uzio wa baharini ili kuzuia uingiaji wa silaha nchini humo. Lakini kutimiza yote hayo, inahitaji msaada wa kifedha kutoka Umoja wa Mataifa. Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameuunga mkono mpango huo kwa sauti kubwa, lakini bado hawajatosheka na maelezo na sasa wanataka ufafanuzi zaidi.

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jijini New York, MarekaniPicha: picture alliance/dpa

Akiongea na waandishi wa habari mjini New York hapo jana (21 Oktoba 2010), Kamishna wa Umoja wa Afrika anayehusika na Amani na Usalama, Ramtane Lamamra, amesema kwamba Baraza la Usalama linataka kujua ni vipi na vikosi vipi vya kuweza kufikia malengo ya kisiasa kabla ya kuidhinisha mpango huo.

Mjumbe mwengine wa Kimagharibi, ambaye alishiriki mkutano huo wa nchi 15 wanachama wa Baraza la Usalama, amesema kwamba wanachohitaji ni maelezo ya kina zaidi na kwa hivyo waliotoa pendekezo hilo wametakiwa kuupitia tena mpango wao na kurudi na ithibati ya kile wanachokiomba.

Uganda, ambayo tayari ina wanajeshi wengi zaidi kwenye kikosi cha AMISOM, ilishasema kwamba inaweza kupeleka wanajeshi wote 20,000 wanaohitajika na mpango huo wa Umoja wa Afrika, ikiwa tu watagharamikiwa na Umoja wa Mataifa.

Juzi (20 Oktoba 2010), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Johnnie Carson, alisema kwamba nchi yake inaunga mkono mpango huo wa Umoja wa Afrika, lakini hakutaja ni idadi gani ya walinda amani ambayo nchi yake inakubaliana nayo.

Tayari Umoja wa Mataifa unachangia dola za Kimarekani milioni 130 kila mwaka kwa kikosi cha AMISOM na baadhi ya wanadiplomasia wa Kimagharibi kwenye Umoja huo wanaona kuwa kiwango cha wanajeshi 20,000 ni kikubwa sana, lakini wanatabiri uwezekano wa makubaliano ya idadi halisi.

Kuhusiana na suala la kutenga eneo ambalo ndege haziruhusiwi kuruka na uzio cha baharini, Lamrana alisema kwamba linaungwa mkono, lakini kwa sasa bado halijapewa uzito mkubwa. Alisema kwamba anatarajia Baraza la Usalama litapitisha azimio la kuidhinisha ongezeko la walinda amani wa AMISOM mwezi Februari mwakani, vikosi hivyo vitaanza kuwasili Somalia.

Kwa muda mrefu, Umoja wa Afrika umekuwa ukiutaka Umoja wa Mataifa kutuma vikosi vyake wenyewe vya kulinda amani nchini Somalia au kuvipa hadhi vikosi vya AMISOM kuwa vya Umoja wa Mataifa, lakini inaoenekana kumbukumbu za matukio ya miaka ya 1990, ambapo wapiganaji wa Kisomali waliwauwa na kuwaburuza barabarani wanajeshi wa Marekani zinaendelea kuwa kikwazo.

Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Usalama, Lamrana aliilaumu jumuiya ya kimataifa kwa kile alichokiita "kujihusisha kwake nusu nusu na hatua zake za mguu ndani mguu nje kwa matarajio ya uongo kwamba mgogoro wa Somalia unaweza ukatatuliwa."

Ombi lake la kutaka kukijenga kikosi cha AMISOM liliungwa mkono na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon ambaye alisema kwamba hatua za kupambana na waasi nchini Somalia zinaonesha mafanikio na hivyo kulitaka Baraza la Usalama kufanya "maamuzi ya kishujaa na ya kijasiri".

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters

Mhariri: Josephat Charo