1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yasema watu milioni 820 wanakabiliwa na kitisho cha njaa

10 Juni 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka hatua za haraka zichukuliwe ili kukabiliana na kitisho cha njaa duniani. Guterres amesema kiasi cha watoto milioni 144 chini ya umri wa miaka 5 wamedumaa

https://p.dw.com/p/3dZ0E
Antonio Guterres PK Covid-19
Picha: webtv.un.org

 

Ni kinaya kikubwa kwamba kuna chakula cha kutosha cha kulisha watu bilioni 7.8 duniani kote lakini mifumo ya chakula inashindwa kufanya hivyo, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Guterres aliyezindua mkutano wa kujadili kuhusu athari za ugonjwa wa Covid-19 juu ya usalama wa chakula duniani amesema janga la virusi vya Corona limesababisha idadi ya watu wanaokabiliwa na kitisho cha njaa kuongezeka.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka maradufu kabla ya mwisho wa mwaka huu. Ameongeza kusema watu wengine milioni 49 huenda wakatumbukia katika umaskini kutokana na athari za ugonjwa wa Covid-19.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa katika mkutano huo, ni kuwa hatua za kukabiliana na athari za ugonjwa wa Covid-19 kama vile vizuizi vya mipakani na usitishwaji wa shughuli za kiuchumi kwa kiasi fulani zimeathiri usambazaji wa chakula duniani.

Arif Husain ambaye ni mchumi mkuu katika shirika la mpango wa chakula duniani WFP amesema "Covid-19 imesababisha hali ilivyo sasa kuwa mbaya zaidi. Kwetu sisi, kitu muhimu kabisa ni kuhakikisha kuwa tunawafikia watu ambao wameathirika zaidi na makali ya njaa hata kabla ya ujio wa ugonjwa wa Covid-19."

Covid 19 imesababisha bei ya vyakula kupanda

BG Pink Lady Food Photographer of the Year 2020 | K M Asad
Watoto wakipanga foleni katika kambi ya wakimbizi ya Ukhiya ili kupokea chakula cha msaada Picha: K M Asad

Naye mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa kwenye mkutano wa kujadili kuhusu usalama wa chakula uliopangwa kufanyika mnamo mwaka 2021, Agnes Kalibata amesema mazao ya chakula kutoka Marekani hadi India yanaoza mashambani kutokana na vizuizi vilivyowekwa nchini humo.

Kupitia taarifa, Kalibata amesema hali hiyo imesababisha bei ya vyakula kupanda. Vile vile ukosefu wa ajira, kupungua kwa mapato kumefanya upatikanaji wa chakula kuwa mgumu zaidi.

Mjumbe huyo maalum wa Umoja wa mataifa ameongeza kusema mamilioni ya lita za maziwa zinamwagwa Uingereza kwa kukosa wanunuzi ilhali nchini Colombia, familia zinalala njaa.

Kalibata amesema kuwa nchi zinakabiliwa na maamuzi mawili magumu, aidha kuchagua kuwaokoa watu dhidi ya Covid-19 au kuwaacha wafe kutokana na njaa.

Ili kukabiliana na hali hiyo ya ukosefu wa chakula wakati wa janga la virusi vya Corona, Guterres amesema kuwa vyakula na huduma za lishe bora zinapaswa kuwekwa katika orodha ya vitu muhimu.

Vile vile, ameongeza Guterres, nchi zinafaa kuhakikisha upatikanaji wa chakula unakuwa rahisi hasa kwa makundi ya watu walio hatarini zaidi kama vile watoto, wanawake waja wazito na wazee.