1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMyanmar

UN yapitisha azimio la kumalizwa kwa machafuko Myanmar

Saleh Mwanamilongo
22 Desemba 2022

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitaka serikali ya kijeshi ya Myanmar kumuachia huru kiongozi aliondolewa madarakani Aung San Suu Kyi.

https://p.dw.com/p/4LJK4
Umoja wa Mataifa wataka Aung San Suu Kyi aachiwe huru
Umoja wa Mataifa wataka Aung San Suu Kyi aachiwe huruPicha: Jürgen Schwenkenbecher/picture alliance

Azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeomba kukomeshwa mara moja ghasia na kuwataka watawala wa kijeshi kuwaachilia huru wafungwa waliozuiliwa kiholela na kurejesha taasisi za demokrasia.

Umoja wa Mataifa umevitaka vyama vinavyopingana nchini kuendeleza mazungumzo na maridhiano na kuzitaka pande zote kuheshimu haki za binadamu, uhuru wa kimsingi na utawala wa sheria.

Nchi wanachama 12 wa Baraza la Usalama zilipiga kura za ndio, na tatu zilijizuia kupiga kura ikiwemo China, Urusi na India.

''Azimio hili linataka kusitishwa kwa ghasia''

Balozi wa Uingereza, iliyotoa mapendekezo ya azimio hilo, Barbara Woodward amesema kupitia azimio hilo kwamba wanapeleka ujumbe mzito kwa serikali ya Myanmar na wanaamini viongozi wa kijeshi watatekeleza kikamilifu.

''Kwa kupitishwa azimio hili, Baraza limeitikia wito wa viongozi wa jumuiya ya ASEAN kwa msaada wa Umoja wa Mataifa kwa juhudi zao. Azimio hili linataka kusitishwa kwa ghasia; utekelezaji wa haraka na thabiti wa makubaliano ya masuala matano ya ASEAN, heshima kwa utashi wa kidemokrasia wa watu wa Myanmar, heshima kwa haki za binadamu, na uwajibikaji kwa wale wanaokiuka haki hizo, ufikiaji kamili na usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu kwa wale wanaohitaji, na kuachiliwa mara moja kwa wale wote waliozuiliwa kiholela, akiwemo Aung San Suu Kyi na Rais Win Myint.'' alisema Woodward.

Pongezi za Marekani

Viongozi wa kijeshi wa Myanmar kushiriki kwenye mazungumzo nchini Thailand
Viongozi wa kijeshi wa Myanmar kushiriki kwenye mazungumzo nchini ThailandPicha: AFP

Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa Zhang Jun alisema alijizuia kwa sababu kauli ya azimio hilo halina usawa. Wanachama 15 wa baraza hilo kwa miongo kadhaa wamekuwa wakitofautiana kuhusiana na suala la Myanmar, lakini waliwahi kukubaliana kutoa taarifa rasmi kuhusiana na Myanmar ambayo imekuwa chini ya utawala wa kijeshi tangu Februari 2021.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, alipongeza kupitishwa kwa azimio hilo kama hatua muhimu lakini akasema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikuwa na kazi zaidi ya kufanya kuendeleza suluhu ya haki kuhusu mgogoro huo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric alisema Katibu Mkuu Antonio Guterres bado ana wasiwasi mkubwa kuhusu kuzorota hali ya kibinadamu na haki za binadamu nchini Myanmar. Dujarric ameliambia shirika la habari la AP kwamba katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha azimio hilo kama ujumbe mkali kutoka kwa Baraza la Usalama.

Juhudi mpya za kidiplomasia

Wakati huo huo, mjumbe wa kikanda aliyepewa jukumu la kutatua mzozo wa Myanmar atahudhuria mkutano usio rasmi nchini Thailand siku ya Alhamisi, huku chanzo cha serikali ya Thailand kikionyesha kuwa waziri wa mambo ya nje wa serikali ya Myanmar pia atahudhuria kikao hicho.

Jumuiya ya Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia, ASEAN, hadi sasa imeongoza juhudi za kidiplomasia kutatua machafuko ambayo yameikumba Myanmar tangu jeshi lilipochukua madaraka mwaka jana.