1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

UN yaomba msaada wa kukabiliana na serikali ya Taliban

17 Machi 2023

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limemuomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kutoa tathmini huru ya namna ya kukabiliana na utawala wa Taliban pamoja na changamoto zake.

https://p.dw.com/p/4OpDc
Afghanistan | Taliban Versammlung in Kabul
Picha: Wakil Kohsar/AFP/Getty Images

Baraza hilo lililo na nchi wanachama 15 kwa pamoja lilipitisha azimio linalomtaka Guterres kutoa ripoti katikati ya mwezi Novemba, ikiwa na mapendekezo ya mbinu za kufanya kazi na utawala huo katika nyanya muhimu kama siasa, hali ya kibinaadamu na maendeleo ndani na nje ya Umoja wa Mataifa.

Changamoto nyengine ni ukiukwaji wa haki za wanawake na wasichana, masuala ya ugaidi na hali mbaya ya kiuchumi, matatizo ya kidini na kushinikiza mazungumzo ili kuimarisha utawala bora na  utawala wa sheria nchini Afghanistan.

UN: Afghanistan ni taifa kandamizi zaidi duniani

Utawala huo wa Taliban uliochukua madaraka Agosti mwaka 2021 wakati wanajeshi walioongozwa na Marekani walipoondoka nchini humo, baada ya miaka 20 ya vita, umeendelea kusisitiza kuwa unaheshimu haki za wanawake chini ya sheria zake tata za kiislamu.

Lakini licha ya kusema hivyo, limewapiga marufuku wanawake na wasichana kuendelea na masomo ya sekondari na vyuo vikuu, kutembelea maeneo ya wazi na hata kufanya kazi na mashirika ya misaada ya kiutu. Wanawake pia hawaruhusiwi kuondoka nyumbani bila ya kusindikizwa na jamaa zao wa kiume na ni lazima wafinike nyuso zao.

UN yasema Taliban imeshindwa kutekeleza ahadi zake

Afghanistan Frauen Mädchen Symbolbild
Wanawake wa Afghanistan wakijifunika kama inavyohitajika kisheria Picha: DANIEL LEAL/AFP

Mjumbe wa Falme za Kiarabu UAE kwa Umoja wa Mataifa Lana Nusseibeh amesema Baraza hilo linaangalia kwa makini na kupima majibu yake kwa hali hii ngumu pamoja na wataalamu kutoka nje, lakini kile inachoweza kusema ni kwamba hatua ya kufanya kazi kama kawaida na kundi la Taliban sio wazo zuri.

Umoja wa Mataifa waionya Ulaya dhidi ya kusitisha msaada Afghanistan

Amesema anatumai mapendekezo yatakayotolewa na Gutteres yatasaidia kutanua mawazo ya baraza hilo pamoja na Jumuiya ya Kimataifa katika suala hili tete la Afghanistan. Lana Nusseibeh amesema kwa sasa hakuna mkakati wowote wa kimataifa wa kupambana na changamoto ya serikali ya Taliban.

Hata hivyo Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa lilielezea wasiwasi wake kwa Utawala huo kushindwa kuendelea na utekelezwaji wa ahadi zake. Pia lilihimiza umuhimu wa kuheshimiwa kikamilifu haki za wanawake, wasichana, watoto, watu waliowachache na hata watu walio katika mazingira magumu.

Huku hayo yakiarifiwa, Umoja wa Mataifa umeomba dola bilioni 4.6 mwaka 2023 ambacho ni kiwango kikubwa zaidi kuweza kuomba na umoja huo kuisadia nchi moja. Fedha hizo zinatarajiwa kusaidia kupeleka misaada nchini Afghanistan ambapo inasemekana thuluthi mbili ya idadi ya watu nchini humo ambayo ni sawa na watu milioni 28 wanahitaji msaada wa dharura.

Chanzo: Reuters/ap